BARAZA LA FAMASI SIMAMIENI TAALUMA KWA WANANCHI:RAS MWANZA
Bodi mpya ya Baraza la Famasi nchini imeshauriwa kusimamia vizuri taaluma kwa wananchi ili kuepusha madhara yanayoweza kuepukika ya utumiaji wa dawa kiholela bila kufuata misingi sahihi.
Mbali na hilo Bodi hiyo pia imetakiwa kuimarisha ushirikiano na Ofisi ya mkuu wa mkoa pamoja na kuweka utaratibu wa kuhakiki dawa mara kwa mara ili mtumiaji awe salama wakati wote.
Rai hiyo imetolewa leo Septemba 9,2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza,Ndugu Balandya Elikana alipofanya mazungumzo mafupi na uongozi wa Bodi hiyo Ofisini kwake ikiongowa na Mwenyekiti wake Bw.Jaffari Liana na Msajili Boniface Magige walipofika kujitambulisha.
"Hongereni kwa uteuzi wenu wa hivi karibuni,ni imani yangu mnakuja na mageuzi chanya kwenye eneo lenu mkizingatia mnahusika na jambo nyeti katika maisha ya mwananchi la utumiaji wa dawa kwa usahihi.
Balandya amebainisha sehemu nyingi kwenye duka za dawa anakuwepo muhudumu ambaye hana taaluma husika hali ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu.
"Wekeni mkazo wa mtu anayekuja kununua dawa awe na cheti chenye maelekezo ya Daktari hii itaepusha kutoa dawa kwa mtu anayekwenda kufanyia matumizi yasiyo lengwa,"amesisitiza mtendaji huyo wa Mkoa.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bw.Jaffary Liana amebainisha ujio wao ni ziara wanaofanya kwenye Ofisi zao zote za Kanda kujionea shughuli zao na kutoa maelekezo.
"Tukiwa mkoani hapa tutakutana pia na Wafamasia wa Mkoa na kupeana maelekezo yote ya kitaalamu ili kuhakikisha kunakuwepo na muendelezo wa utoaji wa huduma bora kwa mwananchi,"Boniface Magige,Msajili wa Bodi
Jukumu la msingi la Baraza la Famasi nchini ni kusajili wanataaluma wa fani ya famasi pamoja na kusimamia utendaji kazi wao katika maduka ya dawa na hospitali za umma na binafsi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.