Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba limetoa miezi mitatu kwa watumishi waliolipwa fedha Tshs Milioni 52 bila vithibitisho, Tshs Milioni 84.1 za Mishahara kwa watumishi waliostaafu na Tshs Milioni 126.5 za Msaada wa Chakula zilizokusanywa na kutotumwa Ofisi ya Waziri Mkuu kinyume na taratibu kurejesha fedha hizo.
Hayo yamerjiri leo Juni 22, 2022 wilayani Kwimba wakati Baraza Maalumu la Madiwani la Halmashauri hiyo lilipokutana kujadili Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali kwa Mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2021.
"Hatukubali kulea uzembe popote ilipo fedha ya umma lazima irudi, hata kama aliyekula amehama akatwe kwenye mshahara wake na kama amestaafu akatwe kwenye pensheni yake ili fedha za Serikali zirudi hapa." amesisitiza Mkuu wa Mkoa Mhe. Mhandisi Robert Gabriel.
Katika wakati mwingine, Mkuu wa Mkoa ameagiza vyombo vya usalama kuwahoji wataalamu watatu waliohusika kusimamia ujenzi wa jengo la Kantini lililo katika hatua za chini za utekelezaji na kukwama kukamilika kwa zaidi ya miaka 5 hata baada ya kutumia Tshs Milioni 113 kati ya Milioni 160 zilizotengwa.
"Ukimya kwenye mahala ambapo fedha hazitumiki vizuri ni doa kubwa sana ni lazima mpaze sauti kukemea na waliotumia vibaya fedha za umma lazima muwataje na msiruhusu uovu uote mizizi tena," amesema Mkuu wa Mkoa wakati akisisitiza kutolega kwenye kuchukua adhabu kwa wabadhirifu.
"Mkurugenzi lazima uhakikishe kila Mkuu wa Idara anajibu hoja zake na usisite kuchukua hatua kwa yeyote atakayechelewa na mwanasheria kuwa makini naona hauijuwi Halmashauri yako, fuatilia kwa karibu ujue kasi zako vizuri na kufanikisha haya yote lazima muwe na ushirikiano" Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike.
Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Mwanza, Waziri Shabani amesema Mwaka 2020/21 Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ilikaguliwa na kupata Hati Inayoridhisha na kuanzia mwaka 2012/13 hadi 2020/2021 Halmashauri hiyo ina jumla ya Hoja 120 ambapo 70 zipo kwenye hatua mbalimbali ya Utekelezaji na 50 zimefungwa.
"Mhe. Mwenyekiti, sababu kubwa ya hoja kutofungwa kwenye Halmashauri hii ni kutokana na Halmashauri kutoweka mkakati thabiti wa kujibu Hoja kikamilifu na Menejimenti kutokua na vielelezo na ushahidi wa kuthibitisha matumizi na malipo mbalimbali yaliyofanyika." Bwana Waziri.
_Mwisho_
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.