Bilioni 699 kujenga daraja Mwanza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.John Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo- Busisi lenye urefu wa km 3.2 ambalo litagharimu bilioni 699.2 pamoja na barabara unganishi ya kiwango cha lami yenye urefu wa km 1.66 za kiwango cha lami.
Daraja hilo ambalo linajengwa katika Ziwa Victoria litaunganisha Mikoa ya Mwanza na Geita na kurahisisha usafiri kwa wakazi wa Mikoa hiyo na maeneo yote wanaotumia njia hiyo na ni kubwa nchini na Afrika Mashariki huku likiwa la 6 Afrika.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi huo ambao unatekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation(CCECC).
Mhe.Dkt.Magufuli alisema,fedha za ujenzi wa daraja hilo zinatokana na kodi za wananchi na litakapo kamilika litakuwa chachu katika shughuli za uchumi na uzalishaji ikiwemo kilimo,uvuvi,biashara na Utalii pia ni muhimu katika maendeleo na kujikwamua kiuchumi kwa wakazi wa maeneo hayo.
"Fedha za ujenzi wa mradi huu ni za kwetu wenyewe kupitia makusanyo ya kodi mnazolipa wala hatujaomba msaada mahali popote,hivyo nawataka mtembee kifua mbele kwani Tanzania siyo maskini bilioni 699.2 karibu bilioni 700 na bado bilioni 300 ifike tirioni 1,tukiamua tunaweza,daraja hili ni muhimu kwa maisha ya wanamisungwi,Sengerema Tanzania na nchi za jirani kwani kuna watu ambao wamepoteza maisha hasa kipindi cha nyuma kutokana na kutumia mitubwi kuvuka wakati kivuko kilipopata hitilafu na wengine wanapochelewa kivuko kutoka Sengerema na maeneo mengine wakiwa wanaenda hospitali ya Bugando kwa ajili ya kupata matibabu," alisema Mhe. Dkt.Magufuli.
Hata hivyo alisema,mradi huu ni muhimu katika maendeleo ya Misungwi na Sengerema endapo wakazi wake watautumia vizuri,hivyo aliwahimiza vijana wa maeneo hayo kujitokeza kufanya kazi na wasikubali watu kutoka maeneo mengine ndiyo wafanye kazi katika mradi huo huku mama lishe na wananchi kwa ujumla wakiutumia kwa kufanya biashara.
Mhe.Dkt.Magufuli alisema,wale wote ambao mradi umewafuata watalipwa fidia kwani zaidi ya bilioni 3.145 zimetengwa kwa ajili hiyo na watakao lipwa ni wale tu wanaohusika na eneo la ardhi siyo majini.
"Uongozi wa Mkoa wa Mwanza hakikisheni wananchi wa maeneo yanayozunguka mradi huu mnawapa kipaumbele cha ajira wakati ujenzi wa daraja hili,na mtakaopewa nafasi fanyeni kazi na siyo kuiba vifaa,ni wasihi watanzania kulipa kodi kwani tukipata fedha zetu tunaweza kufanya mambo yetu wenyewe," alisema Dkt.Magufuli.
Aidha aliwataka,wakandarasi hao waharakishe mradi huo haraka ikiwezekana wafanye kazi usiku na mchana ili ukamilike kwa wakati au kabla ya muda kwani ni muhimu sana kwa nchi na maisha ya watanzania.
Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe.Mhandisi Isaack Kamwele alisema,mradi huo utatumia miezi 48 ( miaka 4) kukamilika ambapo barabara unganishi ya daraja hilo ni sehemu ya barabara kuu ya usagara ambayo inaunganisha Mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani kama Uganda,Congo na Rwanda.
Mhandisi Kamwele alisema,daraja hilo litasaidia kuondoa kero ya wananchi ya kutumia muda mrefu kusafirisha mizigo na abiria wakati wa kuvuka eneo hilo la Ziwa Victoria kati ya Kigongo -Busisi pia kuimarisha usalama huku uboreshaji na ujenzi wa miundombinu nchini ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 na maono yake ya mwaka 2025.
Naye Mtendaji wa Mkuu wa TANROAD Mhandisi Patrick Mfugale alisema,kuanzia wiki ijayo wataanza kutoa fidia kwa wananchi ambao wamepitiwa na mradi huo ambapo ujenzi wake utakuwa bora ambao utadumu kwa miaka mia ijayo.
Aidha mmoja wa wananchi wa Misungwi Neema Emmanuel alisema,endapo daraja hilo litakamilika litawasaidia katika kufanya shughuli zao za kiuchumi na kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine kwani anaamini pia kutakua na uanzishwaji wa daladala ambao utakuwa na gharama nafuu na kuchukua muda mchache pamoja na kuwa na uhakika wa kusafiri wakati wote kwa kuvuka eneo hilo la maji tofauti na sasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.