Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewahimiza wananchi wa mkoa huo kuchangamkia mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kujihakikishia huduma bora za afya wakati wote.

Ameyasema hayo alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kayenze, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwa na maandalizi ya kiafya mapema.

RC Mtanda amesema mpango huo unamlazimu kila mwananchi kuchangia kiasi cha shilingi laki moja na elfu hamsini (150,000) kwa mwaka, kwa familia yenye hadi watu sita. Amesema gharama hiyo ni ndogo ukilinganisha na faida kubwa zinazopatikana kupitia bima hiyo.

Ameeleza kuwa kifurushi cha bima hiyo kinajumuisha huduma zaidi ya 372 za afya, jambo linalowezesha familia kupata matibabu mbalimbali bila mzigo mkubwa wa kifedha wakati wa dharura.

Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga na bima hiyo pindi fursa itakapopatikana, akisisitiza kuwa afya ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa mahitaji muhimu kwa binadamu ni chakula, afya na makazi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anajilinda kiafya kwa kukata bima ya afya kwa ajili ya ustawi wa maisha yake na familia yake.

Akijibu hoja ya barabara iliyowasilishwa na Diwani wa kata hiyo, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa baada ya muda mfupi ujao barabara ya Kayenze itaanza kutengenezwa ili kuboresha miundombinu ya usafiri katika eneo hilo. Aidha, amegusia suala la umeme kwa kueleza kuwa maboresho makubwa yanaendelea kufanyika, na mara baada ya kukamilika hakutakuwa tena na adha ya kukatika-katika kwa huduma ya umeme kwa wananchi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.