BODABODA ALIYEGONGA GARI LA RC MWANZA ANUNULIWA PIKIPIKI MPYA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amekabidhi rasmi pikipiki kwa Bwana Kusan Alex Lumambo Bodaboda aliyesababisha ajali kwenye gari la Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza maeneo ya Mkuyuni Jijini Mwanza tarehe 31 Oktoba, 2024.
Akizungumza mara baada ya kumkabidhi pikipiki hiyo leo Desemba 24, 2024 Mhe. Mtanda amesema yeye ni muumini wa sheria na kijana huyo ndio aliyekuwa na makosa, lakini alihakikisha anamhudumia kwa kulipia gharama za matibabu ya jumla ya shilingi milioni 12.
“Sasa matukio kama haya yanapotokea mara nyingi wadogo wanaamini wanawaonewa na wakubwa, sasa mimi nimetaka kuwaambia wakubwa hawana haja ya kuwaonea wadogo”. Mhe. Mtanda.
Aidha, Mhe. Mtanda kama mlezi wa bodaboda Mkoani humo ametawaka bodaboda kuendesha pikipiki kwa nidhamu na kwa kuzingatia sheria za nchi kwani ajali zinaepukika na wasiwe na haraka kwani haraka sio nzuri.
“Sasa waendesha pikipiki wengine ningependa hii iwe funzo kwamba angalieni gharama hii yote, je mtaiweza? huo ndio ujumbe wangu”. Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
"Kwa hiyo pikipiki ni ajira, ni sekta isiyo rasmi na sisi Serikali tunaitambua na ni lazima nyie wenyewe muijali na kuipenda lakini mjue kabisa mkisababisha ajali za kujitakia mtajikuta matatani." Ameongeza RC Mtanda.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa chombo hicho Kijana Kusan amesema anashukuru kwa kupewa chombo hicho pamoja na msaada wa matibabu licha ya yeye kuwa na makosa.
Akizungumza kwa niaba ya Waendesha Pikipiki Mkoa wa Mwanza Mwenyekiti wa Waendesha Pikipiki Mkoa Bwana Mohammed Iddi amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa moyo wake wa uzalendo na ameahidi kumuunga mkono kwa lolote kutoka katika umoja huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.