Umoja wa Waendesha pikipiki Mkoa wa Mwanza (Bodaboda) wamejitokeza kwa wingi jijini hapa kuwachangia damu majeruhi wa ajali ya moto iliyotokea hivi karibuni mkoani Morogoro na kuua watu zaidi ya 90 na kujeruhi zaidi ya watu 40.
Akizungumza na wandishi wa habari mara baada ya kuchangia damu, Mwenyekiti wa Chama cha Bodaboda Mkoa wa Mwanza Jerald Nyembe alisema wao kama bodaboda wameguswa na tukio la ajali lililotokea mkoani Morogoro na hivyo wakaona ni vyema kuungana na watanzania wengine nchini ili waweze kuwachangia ndugu ambao ni majeruhi wa ajali hiyo.
“Tumeitikia wito wa Serikali hasa wa Rais wetu mpendwa Dkt. John Magufuli wa kuwachangia ndugu zetu damu, ambao kwa sasa wana uhitaji mkubwa,” alisema.
Kwa upande wao, Atanas Lugela na Richard George ambao ni boda boda wanaofanyia shughuli zao jijini Mwanza, walisema tukio la ajali iliyojeruhi na kusababisha watu zaidi ya 700 limewagusa sana na hivyo waliona ni vyema wajitokeze kuchangia damu, ambayo licha ya kusaidia majeruhi ya ajali wa mkoa wa Morogoro, itayasaidia makundi mengine katika jamii, wakiwemo akinamama wajawazito, watoto na majeruhi wengine nchini ambao wana uhitaji mkubwa wa damu.
“Nimeguswa na tukio la Morogoro, na nina hofu ya kesho na ndiyo maana nimejitokeza kuchangia damu, naomba watu wengine nchini nao washiriki kuchangia damu,” alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Maabara na Damu Salama Mkoa wa Mwanza Juma Shigella licha ya kuwapongeza bodaboda wa jijini Mwanza kuitikia mwito wa serikali na kujitokeza kuchangia damu, alisema mahitaji ya damu kwa mkoa kwa siku ni chupa 80 kwa siku na kwa mwezi ni chupa 2,400.
Alisema hata hivyo mkoa una uwezo wa kukusanya asilimia 60 tu ya mahitaji na hivyo kuwa na upungufu wa asilimia 40 ya chupa za damu zinazohitajika kimkoa.
Alimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella ambaye kupitia kwake, mkoa uliweza kukusanya zaidi ya chupa 4000 za damu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Damu Salama ambayo kitaifa yalifanyika mkoani Mwanza.
“Nawaomba watu wajenge utamaduni wa kujitokeza kuchangia damu, kwa sababu duniani kote hakuna kiwanda cha kuteng’eneza damu, na damu inapopatikana inawasaidia watu wote katika jamii,” alisema.
Akizungumza kwenye hafla hiyo ya kuchangia damu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza Jumanne Muliro aliwapongeza boda boda hao kwa uamuzi wao wa kujitokeza kuwachangia damu ndugu zao ambao ni majeruhi wa ajali iliyotokea mkoani Morogoro na kwamba wameonyesha kitendo cha ubinadamu na kuwaomba watu, vikundi, asasi na taasisi za umma kuiga mfano wao.
“Zoezi la uchangiaji damu halizingatii chama wala dini, au kabila, nawashukuru sana kwa jambo hilo mlilofanya,” alisema.
Alisema utambuzi uliofanywa na serikali wa kuitambua na kuirasimisha sekta ya bodaboda nchini umepunguza ajali na kuongeza ajira kwa vijana ambapo pia aliwaomba viongozi wa dini na kisiasa kuiga mfano ulionyeshwa na bodaboda hao kwa kujitokeza kuchangia damu.
“ Niwaombe muendelee kuzingatia kanuni na sheria za usalama barabarani ikiwemo kuvaa kofia ngumu na tushirikiane kwa pamoja kuwakemea na kuwabaini watu wanaotumia bodaboda kufanya uhalifu,” alisema Kamanda Muliro.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.