Shule ya Msingi Butimba ‘B’ imeibuka mshindi wa kwanza katika mtihani maalum uliotungwa na Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na maafisa elimu wa Jiji la Mwanza na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ambapo imekabidhiwa zawadi.
Mtihani huo ulifanyika wiki iliyopita kwa kushirikisha shule nne bora kutoka Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela ambazo ni Butimba A na B, Bwiru na Gedeli ambapo matokeo yametangazwa na Afisa Elimu Mkoa, Michael Ligola ambapo alisema lengo ni kutaka kuona shule za kutoka Mwanza zinaingia katika orodha ya shule 10 bora kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba unaotarajiwa kuanyika Septemba 11 na 12, mwaka huu.
Ligola amesema wanafunzi wa Shule ya Msingi Butimba ‘B’ wamefaulu kwa zaidi ya asilimia 100 katika masomo yote, mshindi wa pili ni Butimba A, mshindi wa tatu ni Bwiru na Gedeli imekuwa ya mwisho ambapo amebainisha somo ambalo limeonekana kutokuwa na matokeo mazuri ni Kiswahili.
Ligola alisema kutokana na matokeo hayo yamempa imani shule za Mwanza zitaingia katika orodha ya shule 10 bora kitaifa katika mtihani unaotarajiwa kufanyika huku akitangaza kwamba kuanzia sasa wanafunzi wataweka kambi mashuleni kwa lengo la kuhakikisha kasoro zilizojitokeza zinaondolewa.
Akikabidhi zawadi kwa mshindi wa kwanza hadi wanne, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio, amesema hakuna sababu inayozuia shule za Mwanza kuingia katika orodha ya shule 10 kitaifa kwa kuwa kila rasilimali zipo, hivyo aliwataka wanafunzi kuongeza juhudi na siyo kubweteka na matokeo hayo.
“Mwanza tunatakiwa kufanya vizuri katika mtihani kwa sababu kila rasilimali zipo na nimedokezwa kwamba mtihani mliofanya umetungwa kwa mfumo wa mtihani wa taifa ambao mnatarajia kuufanya Septemba 11 na 12 mwaka huu, hivyo naomba muongeze bidii zaidi kwa siku zilizobaki.
“Hapa mshindi wa kwanza tutamkabidhi mbuzi mmoja tena beberu na fedha taslimu ambazo mtatumia katika kufanikisha mahafali yenu baada ya mtihani wa taifa, mshindi wa pili, wa tatu na wanne tutawapa fedha taslimu lakini kikubwa nawaomba muongeze jitihada, tunataka shule 10 bora na Mwanza iwemo,”alisema.
Hata hivyo Kadio alitoa Sh. 20,000 kwa kila mwanafunzi, kwa wale 10 waliofanya vizuri katika mtihani huo.Pia aliwaahidi walimu wakuu wa Shule za Butimba, Bwiru na Gedeli kwamba changamoto zilizopo katika shule hizo zitafanyiwa kazi haraka ili kusiwepo na kisingizio tena.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Butimba, Dotto Emmanuel alisema shule hiyo kufanya vizuri ni desturi yao na kuahidi kwamba atawashangaza watu kuingia 10 bora kitaifa ingawa haijawahi kutokea.Hafla hiyo imehudhuriwa na maafisa elimu jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela baadhi ya walimu na wanafunzi.
Hivi karibuni Serikali mkoani Mwanza iliweka maazimio 14 kwa walimu wakuu, maafisa elimu wa kata na taaluma ili kuinua ufaulu kwa shule za msingi 2019/2020 ambapo mitihani hiyo ni sehemu ya utekelezaji kwa vitendo kwa wanafunzi wa darasa la saba wanaotarajia kufanya mtihani wa taifa kati ya Septemba 11-12, mwaka huu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.