Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa kutembelea Halmashauri zote za Mkoa ili kutoa elimu kwenye mabaraza ya madiwani juu ya faida na gharama za bima ya afya ya jamii ya CHF.
Mhe.Mongella alitoa agizo hilo kwenye kikao cha ushauri cha Mkoa (RCC)kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi hiyo na kujumuisha wajumbe mbalimbali, na kuongeza kuwa kutohamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya bima za afya ni dhambi.
"Chukua timu yako nenda kwenye Halmashauri zetu zote kaa na CMT wala hatapoteza kitu chochote kwenda kutoa mafunzo kwenye mabaraza ya madiwani,mkatoe uelewa wa suala hili," alisema Mhe. Mongella.
Aliongeza kuwa Ofisi za ma-DMO watoe elimu ili kuwapa wananchi faida za bima ya afya ikiwemo unafuu wa gharama za afya kwani bima ya afya ni mkombozi kwa wananchi.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa alisema wapo kwenye mchakato wa CHF mpya na kumba hawajasitisha CHF ya zamani ikiwemo bei ya kujiunga na mfuko wa bima ya afya ambayo ni sh.10,000.
"Kama kuna aliyesitisha ni makosa, CHF ya zamani inaendelea mpaka hapo tutakapokamilisha maandalizi ya CHF iliyoboreshwa, hakuna barua iliyotoka kwa Katibu Tawala Mkoa ikisimamisha, bado tunaendelea na utaratibu wa zamani "alisema Dkt. Rutachunzibwa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kwimba Mhe. Sharif Mansoor alisema alitaka kukata bima za wananchi zaidi ya 3000 lakini juhudi zake zikashindikana kwa kuwa na mkanganyiko wa gharama kwani awali ilikuwa sh.10,000 ila akaambiwa sh.30,000.
Hata hivyo Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mhe. Renatus Mulunga alisema wameishaanza kutoa elimu kwa wananchi juu ya faida za bima ya afya.
"Kwa Manispaa ya Ilemela tumeisha elimisha wananchi juu ya CHF iliyoboreshwa kwa utaratibu ni watu sita wa familia moja watalipia sh.elfu 30,000," alisema Mhe. Mulunga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.