Mashabiki wahimizwa kudumisha amani, mshikamano na heshima

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mechi ya kirafiki itakayozikutanisha mashabiki wa klabu za Simba na Pamba, itakayochezwa Januari 12, 2026 katika Uwanja wa Nyamagana, Jijini Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 10, 2026, Mratibu wa mashindano hayo, Bw. Mohammed Bitegeko amesema mechi hiyo imeandaliwa mahsusi kuwaleta pamoja mashabiki wa klabu hizo mbili zenye historia na ushawishi mkubwa katika soka la Mwanza na Tanzania.

Amefafanua kuwa lengo kuu la pambano hilo si ushindani wa kawaida bali ni kuimarisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa mashabiki wa Simba na Pamba, huku ikionyesha wazi kuwa mpira wa miguu ni nyenzo ya amani na maelewano.

Aidha, amesema mechi hiyo inalenga kukuza michezo na utalii wa michezo mkoani Mwanza, sambamba na juhudi za serikali katika kutumia michezo kama chachu ya maendeleo ya jamii.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, mechi itasimamiwa na waamuzi wa soka wenye viwango vya FIFA ili kulinda hadhi ya mchezo, kuzingatia sheria na kuhakikisha usalama wa wachezaji pamoja na mashabiki.

Katibu wa Mashabiki wa Simba Mkoa wa Mwanza Bw. Philbert Kabago amesema Simba itawakilishwa pia na wachezaji wake wa zamani wanaoishi mkoani Mwanza, akisisitiza kuwa maandalizi yako katika hatua za mwisho.

Kwa upande wake, Afisa Habari wa Pamba Jiji, Moses William amesema Pamba iko tayari kwa pambano hilo la kirafiki, huku akibainisha kuwa klabu hiyo pia itashirikisha wachezaji wake wakongwe waliowahi kuitumikia timu hiyo.

Kamati ya maandalizi imewahimiza mashabiki wa pande zote mbili kujitokeza kwa wingi, huku wakizingatia amani, nidhamu, heshima na upendo siku ya mechi.

Mechi hiyo inatarajiwa kuwa mfano wa kuigwa, ikionyesha kuwa Simba na Pamba wanaweza kushindana kwa heshima na kuishi kwa amani kama ndugu.

Simba na Pamba – Ushindani wa Kirafiki, Umoja na Amani ya Kudumu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.