Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kushirikiana na viongozi wengine wa wilaya hiyo kumtafuta na kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa Shule mpya ya Mtaala wa Ufundi (Amaali) ili ahakikishe anakamilisha mradi huo mara moja.

Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo leo katika kijiji cha Mungwe Wilayani Misungwi wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya shule hiyo inayogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.6.

Akizungumza katika ukaguzi huo Mhe. Mtanda amesema Serikali haitakuwa na huruma kwa wakandarasi wanaochelewesha au kufanya kazi chini ya viwango vilivyokubaliwa.

“Hakuna huruma kwa watu wanaoichezea Serikali. Baadhi ya wakandarasi wananufaika na fedha za Serikali lakini wanajenga kwa uzembe, kuchelewesha kazi na kufanya ujenzi kwa mazoea yasiyokubalika,” amesisitiza.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto wa elimu ya awali kuanza masomo kwa wakati.

Ameeleza kuwa kati ya watoto 16,840 waliopaswa kuripoti shule, ni watoto 8,264 pekee ndio walioripoti. Vilevile, kati ya watoto 17,671 waliokusudiwa kuanza masomo katika ngazi nyingine, ni watoto 11,057 tu sawa na asilimia 62 ndio walioripoti wilayani humo.

Kutokana na hali hiyo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji kupita nyumba kwa nyumba kuwatafuta wanafunzi ambao bado hawajaripoti ili kuhakikisha wote wanaanza masomo bila kikwazo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.