Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga amekabidhi wizara ya Fedha kilo 325 ya dhahabu, fedha Sh milioni 305 na gari mbili zilizotaifishwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza kutoka kwa wafanyabiashara wanne.
Wafanyabishara hao ambao mali zao zimetaifishwa ni Sajid Abdallah Hassan (28) mkazi wa Ilala jijini Dar es Salaam na Mwanza mtaa wa Pamba A, Kisabo Kija maarufu kwa jina la Mkinda (55) mkazi wa Mwatulole mkoani Geita, Emmenuel Ntemi (63) ambaye alikuwa dereva mkazi wa kijiji cha Mwatulole na Hassan Sajiq Hassan (28) raia wa Pakistan mkazi wa Mwanza mtaa wa Pamba A ambaye ni Mfanyakazi wa duka la kuuza vito.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana May 31,jijini Mwanza katika ofisi za Benki Kuu Tanzania (BOT) tawi la Mwanza kati ya DPP Mganga na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Khatibu Kazungu mbele ya Waziri wa Madini, Dotto Biteko, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella na kamati za ulinzi na usalama wa Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza baada ya kukabidhi dhahabu, fedha na magari hayo, DPP Mganga alisema walihifadhi mali hizo BOT kama sehemu salama wakati wakisubiri maamuzi ya kesi iliyokuwa ikiendelea katika mahakama ya hakimu mkazi Mwanza.
Mganga alisema baada ya hukumu kutolewa na wafanyabiashara waliokamatwa na mali hizo kutokata rufaa,kwa mujibu wa sheria ofisi ya DPP imeamua
“Kwa kuwa wenye mali wamekiri kosa na hakuna rufaa waliyokata na walitiwa hatiani, hivyo mali tayari ni mali ya serikali na kwa mujibu wa sheria ofisi ya DPP inatakiwa kukabidhiwa kwa katibu mkuu wizara ya fedha.
“Leo nakabidhi mali zote kwa mwakilishi wa katibu mkuu wa wizara ya fedha ambaye ni Naibu wa wizara hiyo, Khatibu Kazungu, pia nakukabidhi amri za mahakama kuonyesha mali hizo zimetaifishwa.
“Amri hizo ni ya mahakama ya hakimu mkazi Mwanza inayonyesha kutaifishwa dhahabu kilo 319 pamoja na dhahabu nyingine kilo 5.8 tuliyokamata mkoani Geita hivyo jumla nakabidhi dhahabu kilo 325 pamoja na fedha taslimiu Sh milioni 305 ambazi zilipangwa kutyolewa kwa maaskari wale ambao kesi yao inaendelea,”alisema.
Hata hivyo Mganga alisema vipo vitu vingine ambavyo vilitaifishwa vikiwamo mizani ya kupimia madini ambapo vyote vimekabidhiwa katika wizara ya fedha.
Akipokea mali hizo, Kazungu alisema alishukuru kwa hatua zote zilizochukuliwa kuanzioa kukamatwa dhahabu hadi kesi ilipoamuriwa mahakamani na Serikali kufanikiwa kutaifishwa mali hizo.
“Nimeongea na katibu mkuu wangu wakati nashuka uwanja wa ndege Mwanza, na akanieleza kwamba fedha hizo na mali zote anazihiytaji sana kwa ajili ya kugharamia huduma mbalimbali za kijamii.
“Nashukuru sana kamati ya ulinzi na usalama kwa kazi waliyofanya kwa kushirikiana na ofisi ya DPP,kama wizara tunaahidi fedha hizo zitahudumia jamii kwa ufasaha na kwa mujibu wa vikokotoo vilivyofanyika tumeelezwa dhahabu pekee ina dhamani Zaidi ya Sh bilioni 27,”alisema.
Naye Waziri wa Madini, Biteko, alisema anaipongeza ofisi ya DPP kwa hatua ya kufungua kesi kubwa sana juu ya madini haya, naipongeza mahakama kwa kutenda haki, wito wangu ni kwa wale wachimbaji wanaotorosha madini wajue ni habari iliyopendwa.
“Mfano hawa wafanyabiashara waliotorosha madini haya ya Sh bilioni 27, wangelipa serikali Sh bilioni 1.8 angeendelea kubaki na fedha nyingi sana lakini leo amepoteza Sh bilioni 27 yote pamoja na magari.
“Sisi tunachotaka katika madini ni kulipa asilimia 7.3 pekee hata ukiwa na mabiklioni mangapi tunataka kiasi kidogo sana, utaona katika ukanda wa huu wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania pekee ndiyo inatoza kiasi kidogo sana.
“Tunaomba wafanyabiashara wafuate sheria, ofisi ya DPP na mahakama ziendelee na mwenendo huo huo ili kuokosa rasilimali zetu, hongera waandishi wa habari kwa kutangaza jambo hili kwa kila hatua na leo tunahitimisha kwa kukabidhi mali serikalini.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mongella alipotakiwa kusema chochote, alisema hana cha kusema ila alidokeza kwamba akumbukwe katika mgawo wa fedha hizo maana alikimbia akiwa na sweta wakati akielekea kukamata dhahabu hiyo.
Katiaka sakata hilo la dhahabu lilitokea Januari 4, mwaka huu, liliwahisisha askari E. 4948 CPL Dani Kasala, F. 1331 CPL Matete Misana, G.1876 PC Japhet Lukiko, G.5080 PC Maingu Sorrah, G.6885 PC Alex Nkali, G.7244 PC Timoth Paul na H.4060 PC David Ngelela ambao wamesimamishwa kazi.
Pia aliyekuwa kiongozi mwandamizi wa mkoa wa Mwanza, SSP Moris Okinda ambaye aliongoza kikosi cha kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 700, naye amesimamishwa kazi na ambapo hadi sasa kesi bado inaendelea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.