DKT BITEKO AONGOZA KONGAMANO LA KIKANDA DIRA YA TAIFA 2050 MWANZA
Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Julai 20, 2024 ameongoza kongamano la kwanza kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050 lililofanyika Mkoani Mwanza kwenye ukumbi wa Kwatunza Beach Resort.
Akizindua kongamano hilo pamoja na taarifa ya maendeleo ya watu Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu kutoa maoni ili kumiliki dira itakayofikiwa, kuwahusisha moja kwa moja makundi ya kiuchumi pamoja na kusaidia kukubaliana na changamoto zilizobainika katika utekelezaji wa dira ya sasa.
Aidha, amesema ukuaji na muendelezo wa mageuzi kiuchumi ndani ya nchi yameendelea kuimarika ukilinganisha na tulikotoka kwa wastani wa asilimia 6.1 kutoka mwaka 2000 hadi 2021 na sasa Taifa lipo kwenye wakati muhimu wa kuandaa mpango kabambe wa kuamua tunataka kuishi vipi miaka 25 ijayo.
"Duniani kwa sasa kuna matishio ya maendeleo kama mabadiliko ya tabia nchi, mabadiliko ya kiteknolojia, kidemografia na machafuko ya kisiasa na hatuna budi kuyakwepa na kuweka juhudi na bidii kwenye uandaaji wa mipango thabiti ya kukua kiuchumi". Mhe. Dkt. Biteko.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema mkoa huo wenye watu zaidi ya Milioni 3.6 unachangia pato la taifa kwa Tshs. Trilioni 12.2 huku ukiwa ni mkoa wa pili kwa uchangiaji kwa asilimia 7.1 ukitanguliwa na Dar es Salaam pekee.
"Mkoa wetu umejiimarisha kwenye sekta za viwanda, ujenzi, kilimo, maji, utalii, ufugaji na uvuvi na tunaendelea kuzibaini na kutatua changamoto ili tuendelee kuimarika kwenye uchangiaji wa pato la Taifa na ukuzaji wa uchumi wa nchi." Amefafanua.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo inayotekelezwa mkoani humo kama ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi (Bilioni 716), Reli ya Kisasa (SGR), Vivuko vipya (Bilioni 28), Soko la kisasa la mjini kati (Bilioni 23), mradi wa chanzo cha maji Butimba (Bilioni 79) pamoja na usambazaji (Bilioni 400) na Meli ya Kisasa kwa bilioni 123
Kongamano hilo lililowakutanisha wadau kutoka Mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Shinyanga, Mara na Simiyu limechagizwa na kaulimbiu isemayo "Tanzania Tuitakayo 2050 Dira yako, Dira Yetu".
Aidha wananchi wanaweza kutoa maoni yao kupitia *152*00# bila malipo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.