Makamu wa Rais Mhe.Dk t. Philip Isdor Mpango ameiagiza Wizara ya Ofisi ya RaisTawala za Mikoa na Serikali za Mitaa( OR- TAMISEMI) kuona namna ya kuongeza mabweni katika shule sita za Sekondari zilizopo Jimbo la Kwimba Mkoani Mwanza ili kuwaondolea changamoto ya umbali na vishawishi kutoka kwa wanaume wanafunzi wa kike.
Pia amewaasa wananchi kutunza miundombinu ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ili idumu na kuwahudumia kwa muda mrefu kwani fedha zinazotumika kuijenga ni zao wote kwa kuwa wanalipa kodi.
Mhe.Dkt.Mpango ametoa maagizo hayo leo Aprili 11,2023 wakati akiwasalimia wananchi wa Kata ya Hungumalwa Wilaya ya Kwimba Mkoa wa Mwanza akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.
Mhe.Dkt.Mpango alitoa agizo kwa TAMISEMI baada ya Mbunge wa Jimbo la Kwimba Atlaf Mansoor kuiomba Serikali kujenga mabweni na maabara kwenye shule sita zilizopo Kata ya Hungumalwa ili wanafunzi waweze kulala shuleni waepuka vishawishi mbalimbali vinavyowasababishia kushindwa kuhitimu masomo yao na kutimiza ndoto zao.
Mhe.Dkt.Mpango aliwasihi wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule ili wasome na kupata elimu na utaalamu katika sekta mbalimbali kwa faida ya taifa.
"Ili kujenga taifa la kesho lenye vijana na watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri lazima watoto wetu waende shule pia naomba taasisi binafsi, za serikali na wadau wote wa maendeleo ifundisheni jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora hasa kwa watoto na akina mama wajawazito,"amesema.
Akizungumzia umuhimu wa wananchi kutunza miundombinu, Mhe.Dkt. Mpango amesema serikali imetoa fedha nyingi katika mikoa yote nchi nzima kwa ajili ya miradi ya maendeleo ili iwanufaishe wananchi wake na kuwaondolea changamoto mbalimbali zinazowakabili.
"Viongozi na wananchi wote mshiriki kikamilifu kwenye miradi hiyo, wananchi muitunze na viongozi wa umma muwe waadilifu wa fedha hizo za umma zinazotumika kujenga miradi hiyo ili ijengwe kwa ubora ikiwa na thamani halisi ya fedha zilizotengwa,"amesema Mhe. Dkt.Mpango.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Adam Malima akizungumzia hali ya utoro mkoani humo amesema hadi mwishoni mwa Februari mwaka huu 2023 baadhi ya wanafunzi walikuwa
bado hawajaripoti shuleni lakini uongozi wa mkoa kwa kushirikiana na halmashauri husika wanaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kutatua changamoto hiyo .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.