*Dkt.Mpango azitaka Taasisi za kifedha nchini kushusha riba za Mikopo*
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amezitaka Taasisi za kifedha nchini kufanya uchambuzi wa kitaalamu ili riba za ukopeshaji zishuke kwa lengo Watanzania wengi wanufaike na huduma hiyo ambayo ni chachu ya maendeleo ya Taifa.
Akifungua rasmi wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa leo Mkoani Mwanza, Dkt Mpango amesema Serikali imekuwa ikiendelea kuhimiza Taasisi hizo kupunguza riba lakini kumekuwa na muitikio hafifu hali ambayo inawanyima walio wengi kupiga hatua kiuchumi.
"Ukitazama maeneo kama vijijini ni asilimia 8.6 tu ndiyo wanapata huduma za kifedha, hiyo bado ni ndogo sana ukizingatia huko ndiko eneo kubwa la uzalishaji wa kilimo", amesema Makamu wa Rais.
Amesema, baada ya zoezi la Sensa limeonesha sasa tumefikia idadi ya watu Milioni 61.74 kundi kubwa likiwa ni vijana amezitaka Taasisi za kifedha nchini kubuni mkakati wa kulifikia soko hilo ambalo ni nguvu kazi ya Taifa.
"Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo kuhakikisha kundi la Vijana linawekewa mpango maalum ili liweze kujiajiri ,naimani kupitia wiki hii mmewagusa kwa kuwapatia elimu ya fedha na mkakati wa kuwainua kiuchumi"amesisitiza Dkt.Mpango.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Meja Jenerali Suleiman Mzee ameishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuleta wiki hiyo kutokana na Mkoa huo upo Kimkakati kwa kupakana na nchi jirani na kuwa kitovu cha biashara.
"Jumla ya Taasisi 90 za kutoa huduma za kifedha zimepewa leseni na Saccos 64 pia zimepatiwa leseni,hali hii itaongeza wigo kwa wananchi kunufaika katika shughuli zao za kujiletea maendeleo" amesema Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa.
Akizungumzia malengo ya wiki hiyo Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Chande amesema huu ni mwaka wa pili tangu wameanza kufanya na kumekuwa na muitikio chanya tangu Serikali imefanya maboresha katika Sekta za kifedha nchini.
"Mhe Makamu wa Rais maboresho hayo ni pamoja na kuweka sera rafiki ili sekta ya kifedha iwafikie wengi pia kumekuwepo na Mamlaka nyingi za usimamizi wa fedha zenya majukumu ya kuhakikisha huduma hii inafanyika kitaalamu ili malengo yatimie ya asilimia 80 hadi mwaka 2025 wawe na elimu kuhusiana na huduma za kifedha"Mhe.Naibu Waziri.
Wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa inaandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na wadau wake, Mwanza wakiwa wenyeji wakitanguliwa na Mkoa wa Dar-es-Salaam kulikofanyika mwaka jana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.