Viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali watakiwa kuishi kwa maadili na uadilifu ili kujenga nguzo bora yenye kuleta tija katika kukuza na kuchochea maendeleo ya nchi.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella alipokuwa Akifungua kikao kazi cha maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu iliyofanyika Jijini Mwanza, amesema kufuata maadili siyo matukio bali inapaswa kufanywa kwa maisha ya kila siku .
" Mfano mtu anakunywa hakatazwi lakini kuna sehemu kiongozi kama Mkuu wa Mkoa hupaswi kuwa zaidi ya masaa mawili lakini unakuta mtu anakunywa mpaka anashindana kuzungusha laundi ukiulizwa unasema nalinda kura au naamasisha wananchi huku ndipo wapo wengi tuache tabia hizo na tujidhibiti na kufanya Kazi ipasavyo kama anavyofanya Rais Magufuli ili kuleta maendeleo kwa kasi" amesema Mongella.
Naye Katibu Msaidizi wa maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa Godson Kweka akiwasilisha mada ya maadili amesema madhara ambayo yanawezwa kuletwa na kiongozi asiyekuwa na maadali ni makubwa hivyo yawapasa kutambua uongozi ni dhamana ya kuhakikisha unatekeleza majukumu uliopatiwa kikamilifu.
" Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Uzingatiaji wa ahadi ya uadilifu kwa viongozi na watumishi wa ustawi wa utawala bora na haki za binadamu", watumishi mtambue nafasi mlizopewa ni kwa maslahi ya umma na kuwatumikia wananchi na kutotumia nafasi hiyo kwenda kinyume na maadali wengine wanatumia nafasi zao vibaya kwa kutowajibika,kujihusisha, kuwanufaisha marafiki, ndugu na siyo jamii " amesema Kweka.
Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Emmanuel Stenga akiwasilisha hali ya rushwa kwa mkoa amesema wamekuwa wakitekeleza majukumu ya kisheria ya kuzuia ,kuelimisha na kupambana na rushwa na kutekeleza maagizo ya Rais Magufuli ya kutetea wanyonge dhidi ya vitendo vya dhuluma na visivyo vya kiutu.
Ameongeza kwa kipindi cha Julai 2015 Hadi Juni 2020 kwa dawati la uchunguzi pekee TAKUKURU Mkoa wa Mwanza imekamilisha uchunguzi wa majalada 209,kesi 125 zimefikishwa mahakamani, kesi 62 washtakiwa wametiwa hatiani, kesi 49 washtakiwa wameachiwa huku majalada 30 ya watumishi yaliyokuwa yakichunguzwa wamechukuliwa hatua za kinidhamu.
"Kwa kipindi cha mwaka mmoja wa fedha uliopita,Julai 2019 hadi Juni 2020 TAKUKURU mkoani hapa imepokea taarifa 831 , taarifa hizi zinahusisha makosa ya rushwa,makosa mengine ya jinai ambayo siyo rushwa ,vitendo vya dhuluma, ucheleweshaji ama kunyimwa huduma na haki" anaeleza Stenga.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi Afisi ya Kanda ya Mwanza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora Albert Kakengi amesema dhana ya utawala bora ni pana ambayo inasisitizwa duniani kote kuwa ndiyo msingi utaofikia malengo ya milenia, pia ukuaji wa uchumi utasaidia kupunguza umaskini wa kipato na kuimarisha ubora wa maisha na ustawi wa Jamii na isipozingatiwa itachukua muda mrefu kuyafanya hayo.
Dkt.Jacob Mutash ambaye ni Mchungaji wa kanisa la EAGT Kiloleli na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza Hassan Kabeki akizungumzia suala la maadili na uadilifu walisema viongozi wanapaswa kuwa na hofu ya Mungu na kuyazingatia kwa kutenda yale yaliomema na kuwa na bidii ya kutenda kazi ili kuijenga nchi yenye kuleta nuru kwa watu wote.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.