ENG. CHAGU AMTAKA MKANDARASI UJENZI HOSPITALI UKEREWE KUEPUSHA GHARAMA ZINAZOEPUKIKA
Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Miundombinu Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Chagu Ng'oma amemtaka mkandarasi (Dimetoclasa Real Hope LTD) anayejenga mradi wa hospitali yenye hadhi ya Mkoa wilayani Ukerewe kuepuka gharama zinazoepukika katika utekelezaji wa mradi.
Mhandisi Chagu ametoa agizo hilo mapema leo jumamosi tarehe 15 Machi, 2025 akiwa katika kikao kazi cha tatu cha ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo kilichofanyika katika eneo inapojengwa hospitali hiyo katika kijiji cha Bulamba - Nansio wilayani Ukerewe.
Amesema, vitako vya nguzo katika kuandaa msingi ni lazima kwanza wafanye marekebisho madogo kwa maeneo yenye ardhi ngumu inayohusisha mawe kwa kutochimba na kuharibu miamba ili kupunguza gharama za ongezeko la fedha kwa siku za usoni.
"Mkandarasi tangia tarehe 13 Machi, 2025 umeshapewa fedha za awali zaidi ya shilingi Bilioni 3.7 kwa sasa kazi yako ni kuongeza watenda kazi ili ujenzi uende kwa kasi tunayotaka na hadi juni umalize hatua ya msingi." Mhandisi Chagu.
Aidha, ameongeza kuwa huduma za umeme na maji ziko mbioni kufika kwenye eneo hilo kwa ushirikiano baina ya Mkandarasi, msimamizi wa mradi na mamlaka husika ambapo fedha za kulipia kufikisha mtandao zimeshapatikana.
Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Jesca Lebba ameongeza kuwa idara ya afya ambao ndio wenye mradi wanatamani ujenzi ukamilike kwa wakati sahihi kwa mujibu wa mkataba ili huduma za kibingwa na bobezi zianze kutolewa kwa wananchi wa visiwani humo.
Naye, Mhandisi John Bhoke kutoka kwa Mkandarasi amebainisha kuwa ujenzi umeanza kwa kasi na majengo yote yatakwenda kwa pamoja kwani tayari maeneo yanayohitajika kuchimbwa kwa ajili ya ujenzi wa msingi kazi hiyo imefanyika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.