FURSA ZA UWEKEZAJI KWENYE CHAMA CHA USHIRIKA NYANZA NI NYINGI: MRAJISI
Wito umetolewa kwa wawekezaji wa viwanda, shule, viwanda vya uchakataji Pamba na Vyuo vya ufundi kuchangamkia fursa kwenye Chama cha Ushirika Nyanza NCU ambacho kina maeneo mengi ya kufanya shughuli hizo.
Kauli hiyo imetolewa hivi karibuni na Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Mwanza Bi. Hilda Boniface mara baada ya kufanya zoezi la kukagua na kuhakiki mali zote za chama cha Ushirika Nyanza kwenye baadhi ya wilaya mkoani humo.
Amebainisha kuwa mara baada ya zoezi hilo lililodumu kwa takribani juma moja wapo kwenye mchakato wa kuja na mkakati mzuri wa kuhakikisha fursa zilizopo zinawainua wanachama wake.
Amesema uhakiki walioufanya wamebaini mali zinazotakiwa kuendelezwa, zilizochakaa na maeneo ya kufanyiwa uwekezaji.
"Tumeona baadhi ya mali ambazo zimechakaa na kubaki kuwa mzigo kwa NCU kutokana na kulazimika kulindwa wakati wote, uamuzi utakaofanywa ni kuuzwa, mali zilizo katika hali nzuri ziendelezwe na maeneo mengine yafanyiwe uwekezaji ambao utakuwa na tija kwa wanachama wake kwa mujibu wa maelekezo kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini",amesisitiza Mrajisi msaidizi.
Vilevile amesema majengo waliyonayo yana nafasi ya kufunguliwa vyuo vya ufundi,shule na maendeleo ya viwanda hivyo kuwataka watu kuchangamkia fursa hiyo hasa kutokana na kasi ya uchumi inayozidi kupaa ndani ya Mkoa huo uliopo kimkakati zaidi.
Ameongeza kuwa chama hicho cha Ushirika chenye mali yenye thamani ya shs bilioni 69 na chenye nguvu kuliko vyama vyote nchini,sasa hivi una uongozi imara ambao umejipanga kuwainua wanachama wake kutokana na mapato yatokanayo na chama hicho cha Ushirika
"Zao la Pamba ambalo Serikali imeweka nguvu nyingi kuhakikisha linakuwa mkombozi kwa mkulima bado halifanyi vizuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo tabia nchi,hivyo ni lazima kuwepo na mpango badala wa kumuinua mkulima kwa kumkopesha na kufanya kilimo kingine kama dengu,choroko na jamii ya kunde,"Hilda.
Akizungumzia kuhusu benki mpya ya Taifa ya Ushirika NCB ambayo itazinduliwa rasmi mwezi ujao Jijini Dodoma,Mrajisi huyo wa Mkoa amesema itakuwa mkombozi wa maendeleo kwa wanachama na wasio wanachama wa Ushirika kwani watakuwa na chombo imara cha uchumi kitakacho simamia na kusukuma maendeleo yao.
Chama cha Ushirika Nyanza NCU kilichoanzishwa mwaka 1984 kina jumla ya wanachama 254.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.