Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC) wamefanya ziara ya kukagua miradi yote ya kimkakati katika Mkoa wa Mwanza na kusema kwamba kama kusingekuwapo na katiba, Mhe. Rais Dk.John Magufuli angetakiwa kuendelea kuongoza Tanzania hadi pale atakapoona inamfaa kustaafu mwenyewe.
Pia baadhi ya wajumbe wa NEC walisema itashangaza endapo itatotokea kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) atajitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi ujao wa 2020 kwani itakuwa ni ishara ya kumkwamisha Rais Dk. Magufuli asitimize malengo yake.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Mhe. Humphery Polepole pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe.John Mongella ilianzia ukaguzi wa daraja la juu la watembea kwa miguu la Furahisha, upanuzi wa barabara Makongoro inayoanzia eneo la Ghana hadi uwanja wa ndege wa Mwanza.
Miradi mingine iliyotembelewa ni ujenzi wa jengo la kuhifadhia mizigo (Cargo terminal) katika uwanja wa ndege wa Mwanza, jengo la abiria linalojengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza, jengo na mnara wa kuongozea ndege (control tower) pamoja kipande cha barabara ya mita 500 cha kurukia na kutua ndege kilichoongozwa kukidhi kiwnago cha kimataifa.
Vile vile walikagua karakana ya kampuni ya ujenzi wa meli na vivuko ya Songoro Marine 'Transport Boatyard'ambako kunafanyika ujenzi na ukarabati wa vivuko mbalimbali vya Serikali vikiwamo cha MV Ilemela, Nyerere, Butiama, Chato na vinginevyo.
Pia walitembelea miradi ya ujenzi wa barabara ya Sabasaba hadi Buswelu yenye kilomita 9.7, barabara ya Kisesa-Usagara ya kilomita 16.14, ujenzi wa daraja la pande mbili za Kigongo-Busisi lenye kilomita 3.2 ambalo hivi karibuni liliwekewa jiwe la msingi na Mhe.Rais Dkt. Magufuli ambapo walimalizia ukaguzi wa Bandari ya Mwanza Kusini kuona ujenzi wa chelezo, meli mpya , ukarabati wa MV Victoria na MV Butiama.
Akiwa eneo la Daraja la Furahisha, Mhe.Polepole aliwaeleza wajumbe hao kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwamba baadhi ya fedha za ujenzi wa daraja la Furahisha na upanuzi wa barabara hiyo zilitokana na uamuzi wa Mhe.Rais Dkt. Magufuki kuahirisha maadhimisho ya sherehe za Uhuru na kuelekeza kujengwa kwa miundombinu hiyo.
“Daraja hili na upanuzi wa barabara kutoka Ghana hadi uwanja wa ndege vimejengwa kimkakati, haiwezekani mtu anatua na ndege kisha anakaa kwenye foleni, pia hapa tumejenga jengo la biashara la kimataifa la Rocky City Mall ambapo kuna soko la madini, vile vile kuna uwanja wa mpira wa CCM Kirumba, sasa tunaposema miradi ya kimkakati tunamaanisha kwa vitendo.
“Hii miradi inayojengwa hapa ni kwa faida ya sisi na vizazi vijazo, ipo ambayo tutaanza kuona mafanikio kuanzia sasa lakini mingine wajukuu wetu ndiyo watafaidi na wataelezwa na watoto wetu kwamba ilijengwa na Mhe.Rais Dkt. Magufuli, kwa kasi hii ya miaka minne bila shaka CCM itashinda kwa kishindo 2020 kwa asilimia 100, ushahidi tumeuona kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa,”alisema.
Aidha Mhe.Polepole aliwataka wajumbe wa NEC kuona kazi anayofanya Mhe.Rais Magufuli na kumsaidia kuwaeleza wananchi popote wanapopata nafasi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye alisema kama isingekuwapo katiba inayoweka ukomo wa urais, Mhe.Rais Magufuli anastahili kuongoza Tanzania hadi pale anapoona inastahili mwenyewe.
“Binafsi ni muumini sana kwa wale wanaopendekeza Rais Magufuli aendelee kuwa mpaka astaafu mwenyewe, lakini kwa kuwa kuna katiba inazuia hilo, amefanya mambo makubwa sana na nimekuwa nikiwaza hata ninapokuwa nimelala hivi ni nani ataendeleza miradi hii pale Magufuli atakapostaafu.
Baadhi ya wajumbe wakiwamo Mhe. Antony Diallo, Gasper Kikao, Yasmin Alloo na Jamal Babu walipongeza ujenzi wa miradi ya kimkakati ndani ya Mkoa wa Mwanza ambapo walidai kuwa ndoto ya Mhe. Rais Magufuli hakuna wa kuizuia kwani miradi inayojengwa imejibu kero zote za wananchi.
Waliongeza kuwa miradi hiyo ikikamilika atakuza uchumi wa wananchi, mkoa na taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Songoro Marine, Major Songoro alisema kampuni hiyo imepata mageuzi ya haraka kutokana na Serikali ya awamu ya tano kuipatia zabuni nyingi kitendo kilichofanya kuongeza ufanisi katika kazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.