Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Adam Malima amezitaka Halmashauri zote Mkoani humo kutenga bajeti inayouwiana na mahitaji ili kuwasaidia watoto wa kike kupata taulo na kuweza kuendelea na masomo yao ikiwa ni mpango wa kutokomeza ziro pamoja na daraja la nne kwa wanafunzi wanaoacha masomo yao kipindi cha hedhi.
Amesema hayo leo (Januari 15, 2023) wilayani Magu wakati wa Kikao cha pamoja na Uongozi wa Halmashauri hiyo kilichoketi kujadili kuhusu vigezo muhimu vya kuzingatia hususani katika maandalizi ya bajeti ya Mwaka 2022/23 na kubaini kuwa Halmashauri hiyo ilitenga Shilingi Milioni 7 pekee kwa ajili ya Taulo za kike katika mwaka wa fedha unaoendelea.
"Tatizo lenu hapa mnaweka mpango wa fedha ndogo za kununua Taulo za kike kwa kuwategemea wahisani alafu mkizikosa fedha kwa wahisani mnaadhirika, tuacheni hii tabia ni lazima tuwajali watoto hawa kwani hilo ni hitaji lao la msingi na tutambue kuwa wakiwa na utulivu darasani ndipo hata ufaulu unapanda." Malima amefafanua.
Vilevile, Mhe. Malima amesema kuwa uhai wa Halmashauri unaenda sambamba na uwepo wa fedha za kutekeleza shughuli mbalimbali kwa kadiri walivyojipangia kwenye bajeti hivyo basi ni lazima watendaji wajikite kwenye ukusanyaji kwa mujibu wa sheria ili kuipa Halmashauri uhai.
Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa ameziagiza Halmashauri mkoani humo kuhakikisha fedha zinapelekwa katika utekelezaji wa Mpango wa Lishe kwa kadiri walivyojipangia ili kuwa na kizazi chenye Afya bora hususani kwa watoto wa shule za msingi na sekondari kwani wakiwekewa programu ya kupata uji shuleni itasaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi.
Naye, Katibu Tawala Mkoa Balandya Elikana amezitaka Halmashauri za mkoa huo kuwa na mpango wa kutekeleza Afua za Lishe kwa mujibu wa Mikataba waliyoingia na Mkuu wa Mkoa ili kufanya tathmini itakayosaidia kubaini na kutatua changamoto zitakazojitokeza.
"Haiwezekani kwa wakati huu tukiwa tumebakiza miezi mitano mbele tayari tuwe tumevuka malengo ya Makusanyo tuliyojipangia, hii inaonesha kuwa tuna udhaifu kwenye upangaji wa bajeti zetu na hali hii inaweza kusababisha matumizi mabaya ya fedha." Amesema Katibu Tawala wilayani Magu wakati akifafanua umuhimu wa kuweka bajeti zenye uhalisia.
Vilevile, ameziagiza Halmashauri hizo kuwa na mwenendo mzuri wa Marejesho ya fedha na kusajili vikundi vya wajasiliamali kwenye mfumo kutoka makundi ya Wanawake, Vijana na watu wenye Ulemavu sambamba na kuhakikisha wanafuata miongozo ya utekelezaji kwenye eneo hilo ili marejesho yawiane na ukopeshaji wa fedha.
Katika kuhakikisha mtoto wa kike anakua kwenye Mazingira salama ya kujifunza, Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Salum Kalii amemuagiza Mkurugenzi kuongeza bajeti ya kununua taulo za kike hadi kufikia Milioni 70 hadi 120 ili wanafunzi wa shule za Sekondari waweze kupata huduma hiyo.
Awali, Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Magu Wilbard Bandola alifafanua kuwa kwa mwaka ujao wa fedha wamejipanga kukusanya zaidi kwenye Sekta za Ardhi, Uvuvi, Leseni za Vileo pamoja na Kilimo kwani kuna ishara njema kwenye mavuno ya mazao kama Dengu kutokana na mvua za wastani zinazoendelea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.