HUDUMA YA SCALE KUBORESHA MAISHA KWA WATOTO WANAOISHI NA UGONJWA WA SELIMUNDU
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kupunguza ugonjwa na vifo vinavyosababishwa na Selimundu na kuboresha ubora wa maisha kwa watoto wa Tanzania wanaoishi na ugonjwa huu. Kupitia elimu, uchunguzi wa mapema, kuzuia maambukizi, na msaada wa kisaikolojia wa kudumu.
Akizungumza wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya katika uzinduzi wa mpango wa ujasiri na mabadiliko (SCALE) Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba amesema serikali inakusudia kuhakikisha kuwa kila mtoto aliye na Selimundu ana nafasi ya kukua, kufanikiwa, na kuishi maisha kamili.
Hotuba hiyo imeeleza kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watoto wenye ugonjwa huo ulimwenguni, na inakadiriwa kwamba watoto kati ya 11,000 na 14,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na ugonjwa huo. Katika eneo la Mwanza pekee, karibu watoto wachanga 4,200 huathiriwa kila mwaka.
"Katika nchi zenye mapato ya juu zaidi ya asilimia 90 ya watoto walio na ugonjwa wa Selimundu huishi hadi wanapokuwa watu wazima, hapa Tanzania, asilimia 90 ya watoto walioathiriwa hawaishi zaidi ya utoto".
Ameeleza kuwa Programu ya Huduma ya SCALE inakusudia kubadilisha mwelekeo huo kwa kuunganisha huduma ya ugonjwa huo wa kudumu katika mifumo yote ya huduma ya afya ya msingi. Kupitia uchunguzi wa mapema, hatua za kuzuia na matibabu yanayopatikana, Amesema tutapunguza mzigo kwa hospitali zetu na, muhimu zaidi kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika.
Hotuba hiyo imeeleza, Uzinduzi huo unaashiria mwanzo wa sura mpya ambapo hakuna maisha ya mtoto yatapunguzwa na ugonjwa huo, pamoja kupitia msaada wa washirika wetu na kujitolea bila kuchoka kwa wafanyikazi wetu wa huduma ya afya tutaongeza utunzaji, kuokoa maisha, na kujenga maisha bora ya baadaye kwa watoto wetu.
Seli mundu ni ugonjwa wa kudumu wa mfumo mbalimbali ambao husababisha upungufu wa damu mwilini, kuzimika kwa mishipa ya damu, upungufu wa kinga, na uharibifu wa hatua kwa hatua wa viungo muhimu. Watu walioathiriwa hukumbana na maumivu yasiyoelezeka, viharusi vyenye kulemaza, maambukizo, na kwa kusikitisha wengi hufa kabla ya kufikia utu mzima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.