Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana leo Septemba 22, 2025 amepokea ugeni kutoka wizara ya Katiba na Sheria waliofika mkoani humo kwa ziara ya siku mbili ya kutoa huduma za msaada wa kisheria katika Magereza.
Akiongea na ugeni huo katika kikao kifupi cha kujitambulisha ofisini kwake Bw. Balandya amewakaribisha na kuwatakia kheri katika jukumu hilo muhimu na amewaahidi ushirikiano wakati wote watapokua Mwanza.
Kadhalika, amewasihi kusaidia kupunguza msongamano wa wafungwa na maabusu katika magereza kwa kutimiza wajibu wa kutoa dira ya nini kifanyike kisheria hususani wakati wa upelelezi kuelekea kwenye mwenendo wa kesi.
Kiongozi wa timu hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za Msaada wa Kisheria Bw. Osborn Paiss amesema watakuwepo Mkoani Mwanza kwa siku mbili kwa ajili ya kutoa huduma za Msaada wa kisheria katika magereza ya Butimba, Sengerema na Ukerewe.
Aidha, aeongeza kuwa wizara ya katiba na sheria ipo kwenye ziara ya kutoa huduma za msaada wa kisheria hususani katika magereza yaliyopo katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo wameanza kutekeleza jukumu hilo mkoani Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.