Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)Mhe. Suleiman Jaffo amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi inayofanywa na uongozi wa manispaa ya Ilemela.
Mhe. Jaffo ameyasema hayo muda baada ya kutembelea jengo hilo na kulikagua akiwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Dkt. Severine Lalika, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo John Wanga, watumishi wa Manispaa ya Ilemela na Mhandisi mshauri wa Wakala wa majengo Benard Mayemba.
Mhe.Jaffo alimtaka Mkandarasi anayejenga jengo hilo la utawala kuhakikisha kuwa ifikapo Novemba 30 mwaka huu ahakikishe kuwa jengo hilo ambalo ujenzi wake unafanywa na Wakala wa Majengo (TBA) kupitia kikosi chake cha ujenzi cha BRIGADE kama mkandarasi mshauri uwe umekamilika.
“ Kwa kweli nimefurahishwa na kasi inayiofanywa na Mkandarasi anayejenga jengo hili, ukiliangalia limekidhi viwango niwapongeze sana," alisema Mhe.Jaffo.
Alisema Serikali imetoa kiasi cha Sh. bilioni 38 kwa nchi nzima kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya majengo mbalimbali kwa halmashauri nchini, likiwemo jengo hilo la utawala la manispaa ya Ilemela.
Alimtaka Mkandarasi anayejenga jengo hilo la utawala, ambaye alikuwa amesimama kwa muda kwa sababu ya malipo kuendelea na ujenzi wa jengo hilo na kwamba Serikali italeta fedha za ujenzi wa jengo hilo.
Waziri Jaffo alisema jengo hilo la utawala litakapokamilika litakuwa ni jengo kubwa na zuri la mfano lililojengwa kwa thamani halisi ya fedha kwa halmashauri zote nchini.
Kwa upande wake Mhandisi mshauri wa Wakala wa majengo Benard Mayemba alimueleza Waziri Jaffo kuwa utekelezaji wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 35 na kwamba jumla ya wiki 24 zimetumika kwa ajili ya ujenzi kati ya wiki 52 za mkataba wa ujenzi huo.
Alisema hadi sasa TBA imeishapokea toka kwa Mshitiri kwa niaba ya Serikali Manispaa ya Ilemela jumla ya Sh. 996,793,934.50 malipo ambayo yamefanyika kwa awamu moja ambayo yalilipwa mwezi April mwaka huu ambapo utekelezaji wa mradi ulianza rasmi Mei 6 mwaka huu na kwamba kiasi cha Sh.bilioni 3.8 kinatarajiwa kutumika kwenye ujenzi wa jengo hilo la utawala.
Aidha Muyemba alisema kuwa licha ya juhudi zinachukuliwa na manispaa na wakala katika utekelezaji wa mradi huo, bado mradi huo unakabiliwa na changamoto kuu tatu ambazo ni ukosefu wa fedha kutokana na kutegemea ruzuku ya Serikali, upatikanaji duni wa maji kutoka Mamlaka za maji na uhaba wa vifaa vya ujenzi.
“ Kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji, Wakala kwa sasa unanunua maji kwenye ma-bouza na tayari Mshitiri ameishataarifiwa juu ya tatizo hili, ingawa maeneo haya ulipo mradi huu yanakumbwa na tatizo la jumla la uhaba wa maji,” alisema.
Kazi zinazotekelezwa kwenye mradi huo ni kujenga uzio kuzunguka eneo la mradi, kufanya setting ya jengo, kuchimba eneo la kujengea, matayarisho ya kujenga vitako vya nguzo ukuta wa msingi wa jengo na kumwaga zege la jamvi la chini kwa asilimia 100.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.