Jamii ina mchango mkubwa wa kuutokomeza ugonjwa Ukimwi: RC Makalla
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA. Amos Makalla amesema kazi ya kuutokomeza ugonjwa wa Ukimwi siyo ya Serikali pekee bali jamii bado ina mchango mkubwa wa kupambana nao na kuelimishana kwa njia mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba yake leo Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Seni Ngaga wakati wa Maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika ki-mkoa wilayani humo amesema bado mkazo wa elimu unahitajika kutokana na maambukizi hayo kuchangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo kuendekezwa kwa mila na desturi zilizopitwa na wakati na ngono zembe.
"Mkoa wetu bado unashika nafasi ya juu ya maambukizi ambayo ni asilimia 7.2 hii maana yake bado tuna jukumu kubwa la kuhakikisha kasi hiyo inashuka au inakwisha kabisa," Mhe.Ngaga
Ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Asasi zisizo za Kiserikali zinazopambana na ugonjwa huo na magonjwa mengineyo yasiyoambukiza itaendelea kushirikiana nazo ili kulinda nguvu kazi ya Taifa.
"Wizara ya afya imetoa pia kipaumbele kwa ugonjwa wa homa ya ini ambao umekuwa tishio pamoja na yale yasiyoambukiza, msisitizo wetu ni kuhakikisha jamii inaendelea kujengewa uwezo wa uelewa," Dkt.Florence Nduturu, mwakilishi kutoka Wizara ya afya.
Amewataka wale wote watakaobainika na ugonjwa huo kuanza kutumia dawa kwa usahihi na siyo kutokomea mara baada ya vipimo kuonesha wana maradhi hayo na badala yake kwenda kutumia tiba zisizo sahihi.
Akitoa ushuhuda wakati wa Maadhimisho hayo Deus Sahani anayetokea Baraza la watu wanaoishi na ugonjwa wa Ukimwi, amebainisha hadi sasa ana miaka 16 akiwa na maradhi hayo na amekuwa na afya njema kutokana na kuzingatia unywaji wa dawa kwa usahihi huku akiendelea na shughuli zake za kuipatia familia yake kipato bila tatizo.
"Bado kuna changamoto ya watu mara baada ya kupima na kugundulika wanakwenda kupata matibabu kwa siri na anapokuja kuzidiwa anarudi Hospitali huku akiwa amedhoofika sana na mwishowe kukutwa na mauti", amefafanua ndugu Sahani wakati akihimiza jamii kupambana na ugonjwa huo.
Kila Disemba Mosi Tanzania inaungana na Mataifa mengine Duniani kuadhimisha siku ya Ukimwi huku mwaka huu kauli mbiu ikisema "Jamii iongoze katika kuutokomeza Ukimwi".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.