JAPAN YAJIVUNIA MAHUSIANO MAZURI YA KIDIPLOMASIA NA TANZANIA
Balozi wa Japan Nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa amesema Serikali ya nchi yake imekuwa ikijivunia mahusiano thabiti na imara ya kidiplomasia kati ya nchi hiyo na Tanzania hali iliyopelekea kusaidia kuboresha sekta za miundombinu, afya, kilimo na Uvuvi kwa wananchi wa Tanzania.
Ametoa kauli hiyo leo Oktoba 30, 2024 wakati wa kikao kifupi cha utambulisho na ukaribisho kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kufuatia kuwasili kwake Mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku 2.
Balozi huyo amesema, Japan wanajisikia fahari kuwa sehemu ya uimarishaji wa mifumo ya utoaji huduma bora kwa wananchi wa Tanzania na kuahidi kuhakikisha anasimamia muendelezo wa uhusiano huo mwema wa kidiplomasia ambao umedumu kwa miaka mingi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija amesema Mwanza ni mashahidi wa manufaa ya mahusiano ya nchi hizo mbili kupitia miradi mikubwa inayotekelezwa kwa ushirikiano kama vile masoko ya samaki na miundombinu ya afya.
Mhe. Ludigija ameishukuru serikali ya Japan kwa kuendelea kuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa mkoa huo na kwamba umekua ukichangia kwa zaidi ya asilimia saba kwenye pato la taifa kwa sasa na kuna viashiria vya kuongezeka.
Mhe. Balozi Misawa ametembelea Soko la Samaki la Kirumba pamoja na mwalo wa Mswahili na kesho atatembelea hospitali ya Sumve ambapo atakabidhi jengo la Mama na Mtoto lililojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.