JENGENI MALENGO MAKUBWA KATIKA UFUGAJI WA SAMAKI KWA VIZIMBA:RAS MWANZA
Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amevishauri vikundi vya vijana vinavyojihusisha na ufugaji wa samaki kwa njia ya Vizimba kujenga tabia ya kuwa na mpango biashara ambao utawasaidia kupiga hatua kubwa kiuchumi.
Akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo leo Septemba 18,2024 wilayani Nyamagana,mtendaji huyo wa Mkoa amebainisha bila ya kujiwekea dira katika ufugaji huo itawachukua muda mrefu kupiga hatua.
"Nawapongeza kikundi cha Vijana Agro Group nimesikia taarifa yenu na jinsi mnavyo nufaika kwa kipato,na nidhamu ya marejesho ya mkopo wa asilimia 10, sasa muanze kuwa na mkakati wa kikundi kupiga hatua kibiashara,"amesisitiza Balandya wakati akizungumza na vijana wanufaika na mradi wa vizimba eneo la Luchelele
Aidha amemshauri Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuona namna ya kuwawezesha vikundi vya vijana mtaji mkubwa zaidi kupitia mpango biashara wao kulingana na mapato yao ya ndani ya halmashauri hiyo hali itakayowasaidia katika kupiga hatua zaidi kiuchumi.
Amesema mchakato wa kujengwa kiwanda cha kuchakata chakula cha samaki kipo mbioni kujengwa mkoani Mwanza hali ambayo itapunguza mzigo wa gharama kwa wanufaika
"Tumefanikiwa kupata sh milioni 86 katika mavuno ya samaki mwaka jana na juzi na tumefanikiwa kurejesha shs milioni 22 hadi sasa katika mkopo wa shs milioni 150 tuliopatiwa,"Daisy Ulaya, mnufaika na Katibu wa kikundi cha Vijana Agro Group.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe.Amina Makilagi amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya ufugaji wa samaki kwa njia ya kisasa na kutanua wigo wa ajira kwa vijana.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.