JWTZ KUADHIMISHA MIAKA 60 KWA KUTOA HUDUMA ZA AFYA BILA MALIPO
Luteni Kanali Ahmed Ali Shabhay amewakaribisha wananchi wa Mwanza na Mikoa ya jirani ya kanda ya ziwa magharibi kufika kwenye viwanja vya Furahisha kuanzia tarehe 26 hadi 30 Agosti 2024 kupata huduma za uchunguzi, vipimo na matibabu bila malipo.
Mkuu huyo wa kikosi ametoa wito huo leo Agosti 23, 2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake wakati akielezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na jeshi hilo katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya jeshi hilo mnamo Septemba Mosi, 2024 kufuatia kuasisiwa kwake Septemba Mosi 1964 zikiwemo ya utoaji wa huduma za afya katika hospitali zote za kanda nchini.
Luteni Kanali Ahmed Ali Shabhay amesema jeshi hilo linatokana na wananchi wa Tanzania kwani maafisa na askari wa JWTZ wanatokana na jamii ya watanzania na ni Jeshi lao la wananchi kwa ajili ya kuwalinda na kuwapatia huduma za kijamii wakati wa amani pamoja na majukumu yao ya kiulinzi.
Naye Mkuu wa tiba katika hospitali ya kanda ya jeshi Meja Paul Katema amebainisha kuwa wamejipanga kutoa huduma za upimaji wa magonjwa mbalimbali kama Malaria, Sukari, Zinaa, upimaji wa damu kwa ajili ya uchunguzi wa tezi dume, uchunguzi wa kinywa na meno, saratani ya matiti pamoja na uchangiaji damu.
"Katika hospitali yetu tunatoa huduma za wagonjwa wa nje, wanaolazwa, uchunguzi wa kinywa na meno, upasuaji wa kibingwa wa kinywa, koo na masikio, upasuaji wa jumla, upimaji vipimo vya mionzi kama X-ray, Ultra Sound pamoja na CT Scan. " Amefafanua Meja Katema wakati akizungumzia huduma zitolewazo hospitalini hapo.
Vilevile, Sajin Taji Kemilembe Paulo ambaye ni muuguzi na mtaalam wa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi ametumia wasaa huo kuwakaribisha mabinti na wanawake kufika kwenye hospitali hiyo kupata huduma za uchunguzi wa maradhi hayo zinazotolewa bila malipo.
Daktari wa kinywa na meno hospitalini hapo Meja Simon Mushi amesema watatoa huduma za uchunguzi pamoja na elimu kwa ujumla ya afya ya meno na akatoa wito kwa wananchi kwenda kupata fursa hiyo na akabainisha kuwa ulaji wa vyakula vyenye sukari pamoja na usafishaji usiyo sahihi wa meno vinachangia matatizo ya kinywa.
Halikadhalika, meneja wa Maabara ya hospitali hiyo Kepteni Onesmo Kateule amesema watatoa huduma za vipimo ikiwemo upimaji wa homa ya ini, maambukizi ya HIV, uchunguzi wa tezi dume, sukari, uwingi wa damu, kaswende na watakaohitajika kutibiwa mara moja basi watapata matibabu viwanjani hapo bila malipo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.