Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma imefanya ziara kwenye mradi wa ujenzi wa Daraja la JPM( Kigongo- Busisi) Mkoani Mwanza na kuridhishwa na maendeleo ya utekelezwaji wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Jerry Silaa ameyasema hayo leo Machi 25,2023 baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaogharamiwa na Serikali kwa asilimia 100 kwa gharama ya Sh bilioni 716.33 na kufikia asilimia 70 ya utekelezwaji.
Mhe. Silaa amesema mradi huo unajengwa kwa fedha za serikali ili kuwanufaisha wananchi hivyo wahusika wote wanaousimamia ikiwemo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania(Tanroads) wahakikishe unakamilika kwa wakati, wananchi waweze kuutumia na kupunguza muda wa kuvuka Ziwa Viktoria kwa dakika nne badala ya saa mbili wanazozitumia sasa.
"Nasisitiza tena daraja hili linajengwa kwa fedha za serikali tunaomba likamilike Februari 2024 kama ilivyo kwenye mkataba ili wananchi wanufaike nalo lakini pia tunaipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hakika inafanya kazi kubwa tumekagua mradi huu na mingine ambayo inatekelezwa kwenye mikoa mingine tumepata moyo kwamba nchi hii inajengwa na inafunguka kiuwekezaji,”amesema Mhe. Silaa.
Aidha Mhe. Silaa ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha miradi yote inaendelea kutekelezwa.
“ Hakuna mradi uliosimama na maendeleo yote yanayofanyika yanafanyika katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM),"amesema Mhe. Silaa.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Balozi Mhandisi Aisha Amour amesema hawataongeza muda kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo hivyo ahakikishe unakamilika kwa wakati na ukiwa na ubora kama ilivyo kwenye mkataba.
“Namwagiza mkandarasi ahakikishe mraadi huu unakamilika kwa wakati maana haujawahi kukwama kwa kukosa fedha hivyo tunatarajia ifikapo Februari 24, 2024 atakuwa ameukamilisha ili wananchi ambao wameusubiri kwa muda mrefu waanze kuutumia.
“Pia tunawashukuru sana wabunge kupitia kamati hii ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kufika hapa kwenye mradi kuutembelea na kuukagua maana mnawawakilisha wananchi hivyo wakisikia kutoka kwenu watajua kwamba kazi inaendelea tunawaahidi kwamba utakamilikakwa wakati maana tumekwishamsisitiza mkandarasi azingatie muda" amesema Mhadisi Amour.
Awali akitoa taarifa fupi ya Mkoa wa Mwanza kwa wajumbe wa Kamati hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Paul Chacha ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, alisema ujenzi wa mradi wa daraja la JPM ukikamilika utasaidia kuchochea maendeleo ya ukanda wa ziwa pamoja na taifa kwa ujumla, utaunganisha barabara kuu ya Usagara-Sengerema katika Ziwa Viktoria na mikoa ya Magharibi pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Uganda.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.