KAMBI YA MAGONJWA YA MASIKIO, PUA NA KOO YAZINDULIWA RASMI SEKOU TOURE
Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali watu Bw. Daniel Machunda amezindua utoaji wa huduma ya masikio, pua na koo, inayofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure ikishirikiana na jumuiya ya wataalamu wa Magonjwa hayo Tanzania.
Akizindua huduma hizo Novemba 15, 2024 Bw. Machunda amesema kutokana na shida kubwa kwenye jamii wameandaa utoaji wa huduma za Kibingwa na Kibingwa Bobezi za masikio, pua na koo zinazotolewa kuanzia Novemba15 -16 2024.
Ameongeza kuwa huduma hii itakuwa suluhisho kwa wagonjwa wenye changamoto ya masikio, pua na koo na kuwasihi wananchi wajitokeze kwa wingi ili kupata huduma bora na staha kwa ajili ya ustawi mzuri wa wananchi.
Sambamba na hilo Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amesema magonjwa hayo yameendelea kuwasumbua wananchi wengi hivyo amewahimiza wananchi wenye changamoto hiyo kufika katika Hospitali ya Sekou Toure na kupata matibabu.
"Niwaombe wagonjwa wenye changamoto za masikio, pua na koo wafike na wapate matibabu kutoka Kwa Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi wa masikio, pua na koo." Dkt Jesca Lebba
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekoutoure Dkt. Englebert Rauya amemshukuru uongozi wa jumuiya ya wataalamu wa magonjwa ya masikio, pua na koo Tanzania waliofika katika Hospitali ya Sekoutoure kwa kutaka huduma ya matibabu kwa wagonjwa waliojitokeza na kuwahakikishia huduma nzuri na za haraka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.