Kamishna wa Maadili nchini Jaji wa Rufani Mhe. Sivangilwa Mwangesi, amewataka watumishi wa Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kulinda siri za watoa taarifa kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma ili kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.
Aidha, Mhe.Jaji Mwangesi amewataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu wakijiepusha na shughuli zinazosababisha mgongano wa maslahi wanapotekeleza majukumu yao kwani hiyo ndiyo changamoto kubwa inayowakabili.
Jaji Mwangesi,ametoa agizo hilo jijini hapa leo Juni 16, 2022 wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ambayo huadhimishwa Juni 16 hadi 23 kila mwaka.
“Msijinufaishe na taarifa mnazozipata kutokana na nafasi zenu kwa kujinufaisha nyie wenyewe binafsi, ndugu, jamaa au rafiki zenu kwa kufanya hivyo mtakuwa mnakiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995 sura ya 398 ambayo inalenga kuenzi na kudumisha suala zima la utawala bora, kujenga na kudumisha amani na utulivu nchini.
“Mgongano wa maslahi ndiyo changamoto kubwa inayotukumba watumishi wa umma mfano Serikali inaweza kuwa inataka kutoa ajira ambazo bado haijazitangaza lakini wewe mtumishi ukajua unaanza kuwaambia ndugu, jamaa au rafiki zako ili waanze kujiandaa kwa kufanya hivyo unawaondolea wengine ambao hawajajua haki ya kushiriki kupata nafasi hiyo kikamilifu, au kutokana na nafasi yako labda nafasi za ajira zimetoka unamshinikiza yule anayesimamia nafasi hizo kumpa kipaumbele mwanao, ndugu, au jamaa yako, ”alisema Jaji Mwangesi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, alisema ataendelea kutoa kipaumbele kushirikisha jamii nzima kupambana na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.
"Suala la kujenga, kukuza na kusimamia maadili ni jukumu la kila mmoja wetu hivyo nitoe rai kwa jamii nzima tushirikiane sote kwa pamoja katika ngazi zote na hasa sisi tulioshiriki kikao hiki tuwe mabalozi wa kwanza kufikisha ujumbe vizuri kwa watumishi wenzetu ambao hawajapata fursa ya kuhudhuria kikao hiki na kwa jamii nzima.
Kwa mujibu wa Mhe.Mhandisi Gabriel, lengo la kikao hicho ni kuendelea kutambua dhamira ya kuufanya utumishi wa umma kuwa wenye ufanisi ,kuheshimika, watumishi wa umma kufuata sheria ya utumishi wa umma, kanuni pamoja na kuzingatia viwango vya juu vya maadili ili kukuza utu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kuhusu utendaji kazi serikalini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.