KERO YA MAJI MWANZA SASA KUTOWEKA KABISA: RC MAKALLA
*Ampongeza Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi za Miradi ya maji*
*Asema mikakati ipo Mwanza kuwa ya kwanza kuchangia pato la Taifa*
*Miradi yote ya kimkakati ipo mbioni kukamilika na kuzidi kuipaisha Mwanza kiuchumi*
*Ndege ya kubeba Minofu ya Samaki kuanza kutoa huduma hivi karibuni*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Januari 8, 2024 ameipokea Kamati ya kudumu ya Bunge ya bajeti na katika mazungumzo yake amesema kero ya muda mrefu ndani ya Mkoa wa Mwanza sasa kutoweka baada ya kukamilika mradi mkubwa wa chanzo cha maji cha Butimba.
Akizungumza na wajumbe wa kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Daniel Sillo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Makalla amebainisha mradi huo wa Butimba wenye mitambo ya kisasa ambao upo asilimia 100 kukamilika utatoa kwa siku lita milioni 148 kwa siku.
"Mhe. Mwenyekiti wa kamati Mkoa wa Mwanza mradi huu sasa utawanufaisha wakazi wa Nyamagana, Ilemela, Misungwi na Magu, tunaipongeza sana kamati yako kwa usimamizi mzuri wa fedha hizi za bajeti zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi," CPA. Makalla
Akizungumzia kwa ufupi miradi ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa Mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema ukarabati wa uwanja wa ndege utaanza Februari mwaka huu na kukamilika Juni na mizigo ya minofu ya samaki itaanza kusafirishwa kutoka uwanja huo kuanzia Machi mwaka huu badala ya kuanzia uwanja wa Entebe na Nairobi.
"Tayari tumefanya mazungumzo na uongozi wa ATCL kuhusiana na usafirishaji wa mizigo hiyo baada ya kupata usumbufu wa kwenda kuisafirisha mbali na uwanja huu wetu wa Mwanza," amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge Mhe. Daniel Sillo amesema kamati yake imefika Mwanza ikiwa ni sehemu ya majukumu yake ya kukagua miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Serikali ili iweze kujionea maendeleo na changamoto zake na baadaye kutoka ushauri kwa Serikali.
"Tuna kazi ya kuhakikisha mipango yote ya maendeleo ya kiuchumi hapa nchini inatekelezeka kama ilivyokusudiwa tupo Mwanza kukagua mradi wa chanzo cha maji Butimba, Rais wetu amekuwa mstari wa mbele kutafuta fedha na kuzitoa kwa maendeleo ya wananchi hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tuna muunga mkono kwa kusimamia ipasavyo,"Mhe. Sillo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.