KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AMEZIAGIZA SHULE KUTENGA MAENEO YA UPANDAJI MITI
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava amezitaka shule za msingi na sekondari Mkoani Mwanza kutenga maeneo kwa ajili ya kupanda miti kwa ajili ya kuhifandi mazingira na kulinda uoto wa asili ili kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.
Ndugu Mnzava ametoa wito huo leo t Oktoba 07, 2024 wakati akikagua mradi wa upandaji miti katika Shule ya Sekondari Ibondo ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) wamewezesha upandwaji wa miti 1862 yenye thamani ya Tshs. 533, 260.
Sambamba na hilo Ndugu Mnzava ameshiriki upandaji wa miti 500 na ametumia wasaa huo kuwapongeza na akatoa rai kwa shule zingine mkoani huko kuiga mfano huo mzuri kwani Dunia inapitia changamoto ya hewa ya ukaa hivyo ni lazima watoto wajue umuhimu wa kuhifadhi mazingira.
Aidha, amewapongeza shule kwa kutekeleza kwa vitendo agizo lililotolewa na waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira na Muungano la kusoma na mti ambapo inawajenga watoto kusoma wakihifadhi miti kwani kila mwanafunzi anapanda mti na kuutunza wakati wote hadi unakua.
Vilevile, amekagua mradi wa uoteshaji miche ya miti unaotekelezwa na kikundi cha vijana 'wazalendo forest' na ameiagiza halmashauri kuwasimamia na kuwaendeleza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha shule zinanunua miche kwa ajili ya kupanda kwenye vitalu vyao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.