KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE ATOA MAAGIZO UKAMILISHAJI DARAJA LA NGUDAMA MISUNGWI
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava amemuagiza Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza kuandika barua kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na Katibu Mkuu Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kuharakisha upatikanaji wa fedha za kukamilisha ujenzi wa daraja la Ngudama wilayani Misungwi.
Ametoa agizo hilo leo alhamisi tarehe 10 Oktoba, 2024 wakati akikagua daraja hilo linalounganisha wananchi wa vijiji vya Ngudama na Kaluluma kwa thamani ya zaidi ya Milioni 122 kutoka chanzo cha mfuko wa jimbo ambacho kinasimamiwa na Wizara hiyo.
Kiongozi huyo amesema, Mkandarasi (Barizi investiment Tanzania Limited) ameshatekeleza kazi kubwa (88%) tofauti na fedha alizolipwa jambo linalomkwamisha kuendelea na kuchelewesha lengo la serikali kuwaunganisha wananchi wa vijiji hivyo ambao kwa muda mrefu wamekua wakipata adha ya usafiri na usafirishaji wa mazao.
Aidha, amewataka TARURA Mkoani humo kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo kwa kushirikiana na makao makuu yao ili kuhakikisha mkandarasi huyo anapata fedha haraka iwezekanavyo na kuweza kukamilisha ujenzi wa daraja hilo kwani ukianza msimu wa masika mvua zitamkwamisha kuendelea.
Mwenge wa uhuru wilayani Misungwi umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa madarasa 5 na matundu 10 vya vyoo katika shule ya sekondari Mwasonge vilivyojengwa kwa milioni 85 na kuagiza ukamilishaji wa miundombinu iliyobaki ifikapo januari 2025 ili wanafunzi waanze kusoma hapo kwani itawapunguzia umbali wa kilomita 20 kufuata elimu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.