Neema yawashukia wakazi wa visiwa vya Ukara na Ukerewe mkoani Mwanza baada ya serikali kutatua tatizo la usafiri lililokuwa likiwakabili baada ya Mv.Nyerere kuzama, imetengeneza kivuko kipya chenye uwezo wa kubeba abiria 300 ,magari 10 na mizigo tani 100 kilichogharimu billion 4.2.
Kivuko hicho cha Mv.Ukara hapa kazi tu kimetengenezwa na kampuni ya Songoro Marine iliyopo Jijini hapa kimeingizwa ziwani kwa ajili ya kufanyiwa majaribio ili kuanza rasmi safari zake kati ya kisiwa cha UKara kwenda Ukerewe.
Akizungumzia na waandishi wa habari wakati wa kuingiza kivuko hicho majini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano(Sekta ya Ujenzi), Elius Mwakalinga alisema,kivuko hicho kitaanza kazi baada ya siku tatu kwa sasa kinafanyiwa matazamio ya kuona Kama kinaweza kufanya kazi.
" Kivuko hiki kinabeba wananchi ambao serikali inawathamini sana kuanzia maisha yao pamoja na mali zao hivyo tusingependa masuala mengine kama yaliyotokea yatokee tunamuomba Mungu atuepushe lakini ninachokiona kinaingia majini ni kivuko ambacho tumelipia billion Sh.4.2kama.kingenunuliwa nje ya nchi kingegharimu Sh. Bilioni 22 lakini kampuni ya ndani ya Songoro Marine ilikubali kukitengeneza kwa gharama ya hizo" anasema Mwakalinga.
Aliongeza kuwa kivuko hicho kitafanya idadi ya vivuko kufikia 16 katika ziwa Viktoria na kwamba hiyo ni ahadi ya Rais John Magufuli ,na kuongeza kuwa jumla ya Sh. Bilioni 10 zimetumika kwa ajili ya kujenga vivuko mkoani Mwanza Ili kuhakikisha wananchi wanaoishi katika visiwa 38 wanakuwa na usafiri wa uhakika,akitaja vivuko vingine vilivyonunuliwa miaka ya hivi Karibuni kuwa ni pamoja na Mv. Ilemela,Mv. Chato na Mv. Ukara.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Japhet Masele alisema, kwa sasa wana vivuko 30 ambavyo vinafanya kazi katika Maeneo mbalimbali ya nchi, baada ya kivuko hicho cha MV Ukara kuingizwa ziwani kitaendelea kufanyiwa mazoezi na kuhakikiwa na watalaam kwani kukamilika kwa kivuko hicho ni ukombozi kwa wakazi wa Ukara.
Akizungumza baada kuwekwa kivuko hicho majini, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella alisema, ni takriban miaka miwili kivuko hicho kimekamilika hivyo nchi yetu imshukuru Mungu sana kwa kupata kiongozi mahili mwenye maamuzi,maono na anayeguswa na shida za wananchi.
Anasema wananchi wa Ukara sasa wamepata usafiri ambao utakabidhiwa kwao hivi Karibuni pia alipongeza juhudi za Mhe.Rais John Magufuli kwa namna ambavyo anawasaidia wananchi wa visiwa vya Ukerewe na maeneo mengine ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Cornel Magembe alisema tangu ilipotokea ajali ya Mv.Nyerere mwaka 2018 wananchi walikabiliwa na shida ya usafiri Kati ya Ukerewe na Ukara
Alisema kwa niaba ya wananchi wa Wilaya yake wanatoa shukurani kwa Rais baada ya kutekeleza ahadi yake aliyoitoa baada ya kuielekeza Wizara ya Ujenzi kuunda kivuko kipya ambacho itatatua changamoto ya usafiri katika eneo hilo .
" Wananchi walikuwa wanaisubili kwa hamu kweli hakika leo Kisiwa chote cha Ukerewe kitakuwa na furaha ambayo haiwezi kuelezeka nimeambiwa tarehe 19 kivuko hiki kitafika Ukerewe hivyo nawaomba wananchi wote wa visiwa vyote wajitokeza kwa wingi kuipokea hakika ni Jambo lenye Neema,tunaishukuru awamu ya tano imetekeleza ahadi zake kwa vitendo" anaeleza Magembe.
Major Songoro ni Mkurugenzi wa Songoro Marine anasema wanaishukuru serikali kwa kuwapatia kazi ,kivuko kipo tayari kwa Sasa kipo kwenye majaribio ya mwisho ili kuhakikisha usalama wake ili kiweze kuanza kutoa huduma kwa wananchi .
" Serikali inapowekeza kwenye vitu hivi vinaenda kujenga uchumi mkubwa sana pia sisi tunafuraha kubwa kuwa miongoni wa kujenga uchumi wa watu wa Ukara na Ukerewe" anaeleza Songoro.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.