Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto (Kivulini) limetoa msaada wa kompyuta mpakato 10 katika vitengo maalum vinashughulikia masuala ya ukatili wa jinsia kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza, Kamanda wa Polisi mkoa huo,Hospitali ya Rufaa ya mkoa –Sekoutoure na Wilaya ya Misungwi.
Makabidhiano hayo yalifanyika kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kivulini, Yassin Ally na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Christopher Kadio ambaye pia aliwakabidhi wakuu wa vitendo husika na kuwataka kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kutekeleza Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto 2017-2022 (MTAKUWWA).
Akizungumza baada ya makanidhiano hayo, Ally alisema lengo la kutoa msaada wa vifaa hivyo ni kutaka kuimarisha mfumo wa data-kazi ili kuhifadhi kumbukumbu za vitendo vya ukatili vinavyotokea ndani ya jamii na kufikia lengo la taifa la kupunguza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Ally alisema amelazimika kutoa msaada huo katika idara hizo kwa sababu katika kufanya kazi ya mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili, alibaini kuwapo na changamoto ya watendaji wa Serikali kukosa sehemu salama ya kuweka kumbukumbu zao ambapo nyingi huandikwa kwenye makaratasi na mara nyingine zinapotea.
“ Vitendo hivi vya ukatili bado ni tatizo kubwa sana, ili kuona ukubwa wake nendeni polisi mkaone mashauri yanayopokelewa lakini mengi yanaishia huko huko katika hatua ya upelelezi na machache ndio yanafikishwa mahakamani lakini yanayopata mafanikio yanaweza kuwa 20 kati ya 100.
“Ndiyo maana kama shirika la Kivulini tumeona katika kutimiza malengo yetu tumekuwa tukishirikiana na polisi, hospitali na Ofisi ya Mkuu wa mkoa , wilaya na idara zake, hivyo tumenunua kompyuta 10 zenye thamani ya Sh milioni 12, namkabidhi Katibu Tawala wa Mkoa ambaye atazikabidhi kwa wahusika, haiwezekani tukawa tunapamba na jambo huku hakuna sehemu ya kuweka kumbukumbu.
Ameongeza kuwa watumishi wa Serikali hasa sekta ya afya bado hawapo tayari kujitokeza kutoa ushahidi mahakamani pale wanapohitajika jambo ambalo linaathiri malengo ya kutokomeza vitendo hivyo, vile vile aliwaomba polisi kuongeza jitihada za upelelezi kwani mashauri mengi yanaishia mikononi mwao.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa huo, Christopher Kadio amesema msaada uliotolewa na Kivulini ni mkubwa ambapo aliwataka wajumbe wa kamati ya ulinzi ya wanawake na watoto ngazi ya mkoa kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuhakikisha wanakomesha vitendo vya ukatili wa ngono, kihisia, kimwili na kiuchumi.
“Hakikisheni sasa mnatanua wigo wa kupambana na vitendo hivi maana mtoto akishafanyiwa ukatili tayari inaathiri ukuaji na malengo yake, sote tunajua mpango wa serikali umejikita katika maeneo nane ya kufanyia kazi ikiwamo kuimarisha uchumi wa kaya, kukomesha mila na desturi mbaya, kuimarisha malezi, kujichukulia sheria, utoaji wa huduma kwa waathirika, kuratibu na kutathimini zoezi hilo.
“Kwa kuwa vitendea kazi vimepatikana, utaratibu ni kwamba vikao vya mrejesho vitakuwa vikifanyika kwa kila robo ya mwaka ili kuona mafanikio yake kufikia 2022, naomba kila mjumbe wa kamati ya ulinzi wa wanawake na watoto ya mkoa, aone ana wajibu wa kuleta mbinu ya kumaliza tatizo hili,”alisema.
Naye Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo, Slyvester Ibrahimu, alisema licha ya kuwapo na mapambano ya vitendo vya ukatili lakini takwimu za makosa yaliyoripotiwa polisi yanaonekana kupanda tangu 2016 hadi Juni 2019.
Alisema mwaka 2016 makosa ya unyanyasaji na ukatili kwa watoto yalikuwa ni 1165, 2017 yalikuwa 1287, 2018 ilikuwa1683 na mwaka huu kufikia Juni yameripotiwa 1012.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.