Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amewataka Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine wakiwemo wakuu wa shule za misingi za Serikali Mkoani hapa kujifunza kutoka kwa shule zilizofanikiwa.
Hayo ameyasema alipotembelea Shule ya Msingi Mugini iliyopo Wilayani Magu ambayo imeshika nafasi ya tisa kitaifa kwa matokeo ya darasa la saba.
Amesema kuwa kuna wakati Shule za Serikali zinaendelea kufanya vibaya kutokana na na baadhi ya watendaji wa Wilaya kutokuwa na utayari wa kujifunza kutoka kwa shule zinazofanya vizuri.
"Binafsi nimefurahishwa sana na matokeo ya mtihani wa darsa la saba mwaka huu kwani kwenye kumi bora kitaifa mkoa wa Mwanza umeingiza shule nne Mugini ikiwa mojawapo," alisema Mongella.
"Nimeamua kuwatembelea hapa ili kujua nini siri ya mafanikio kwa sababu mimi nipo tayari kujifunza kutoka kwanu, kwa hiyo niwaombe na viongozi wenzangu ikiwemo wewe Mkuu wa Wilaya ya Magu, ongea nao ili hiyo siri ya mafanikio uipeleke kwenye shule zetu za Serikali.
"Tusione aibu kuwafuata wakatuambia wamefanikiwaje kwa sababu unakuta eti kuna wakurugenzi na wadau wengine wa elimu wanaenda hadi Rwanda kutafuta mbinu ya kuongeza ufaulu wakati watu wa mfano tunao hapa hapa, hebu tuwatumie hawa hawa naamini tutafikia malengo," alisema Mongella.
Awali akisoma risala ya shule hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shule mmoja wa walimu wa Shule hiyo ameeleza kuwa mafanikio ya shule hiyo kitaifa yametokana na juhudi za kila mfanyakazi kutimiza majukumu yake pamoja na huduma bora zinazotolewa shuleni hapo.
"Shule yetu ambayo hadi sasa ina jumla ya wanafunzi 262, kati yao wavulana ni 124 na wasicahana 138, kwa mwaka huu wamehitimu waanafunzi 48 imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza kiwilaya, nafasi ya nne kimkoa na nafasi ya 9 kitaifa.
"Ndugu mgeni rasmi mafanikio haya yametokana na juhudi za kila mtumishi kutimiza majukumu yake pamoja na huduma bora zinazotolewa shuleni kutosheleza mahitaji ya wanafunzi kwa kuwatengenezea mazingira rafiki ya kujifunzia.
"Ingawa tumefanikiwa kuingia kumi bora kitaifa lakini bado kiu yetu kubwa ni kuona kuwa tunaendelea kufanya vizuri zaidi ya hapa na tunaingia nafasi tano za juu na baadaye kuongoza kitaifa ili kuujengea mkoa wetu heshima kubwa.
Hivyo tuuombe uongozi wa wilaya, mkoa hadi ngazi ya taifa kuendelea kushirikiana na shule binafsi ili kuziongezea morali ya kufanya vizuri zaidi na kuzalisha vijana walio na ufaulu bora kabisa,"alisema Mwalimu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Dkt.Philemoni Sengati alisema kuwa wilaya yake inajivunia uwepo wa shule kama hizo zinazoitambulisha kitaifa hivyo ataendelea kuungana na wadau wote wa elimu wilayani humo ili kuleta mafanikio yenye tija zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.