MAADHIMISHO YA WIKI YA MAZIWA KITAIFA YAENDANE NA HADHI YA MKOA WA MWANZA: RAS BALANDYA
*Aitaka kamati ya maandalizi kuhakikisha yanafana na kuwa na tija kwa wana Mwanza*
*Aonesha imani ya mnyororo wa thamani kwa bidhaa ya maziwa kuzidi kuimarika Mwanza*
*Awataka wadau wa maziwa kulitumia jukwaa hilo kuwa wazalishaji bora wa bidhaa hiyo*
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana leo Februari 15,2024 amefungua kikao cha kwanza cha maandalizi ya wiki ya kitaifa ya maziwa itakayofanyika mkoani humo kuanzia Mei 27 hadi Juni Mosi, 2024 na kuitaka kamati ya maandalizi kuhakikisha yanafana na kuwa na tija kwa wana Mwanza.
Akizungumza na kamati hiyo wakiongozwa na ujumbe kutoka Bodi ya maziwa kwenye ukumbi mdogo wa Ofisi ya mkuu wa mkoa, Balandya amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanya uamuzi mwafaka wa maadhimisho hayo kufanyika Mwanza kutokana na Mkoa huo kuzidi kuimarika kiuchumi na kuwa wa pili kuchangia pato la Taifa.
Amebainisha kutokana na hadhi ya Mkoa huo waandaaji wana wajibu wa kuhakikisha maadhimisho hayo yanayofanyika kila mwaka yanaacha fursa nyingi kuanzia kwa mfugaji, mlaji hadi kwa wafanyabiashara wadogo
"Pamoja na lengo la maadhimisho hayo kuboresha na kuhamasisha matumizi sahihi ya maziwa,yatakuwa msaada pia kwa wadau kupata fursa ya kuelimika namna ya kuboresha uzalishaji na kuweza kumudu soko la ushindani kwa ujumla.
Akitoa taarifa fupi kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi,mwakilishi wa Msajili wa Bodi ya maziwa Bw.Aggrey Nsemwa amesema wiki hiyo ya maziwa itaambatana na shughuli mbalimbali kuelekea kilele chake Juni Mosi.
"Ndugu Katibu Tawala mkoa tutakuwa na kongamano kwa wadau wa maziwa lengo likiwa kubadilishana uzoefu na kusikia changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi,pia tutakuwa na zoezi la ugawaji maziwa baadhi ya maeneo ikiwemo kwenye vituo vya kuwalea wazee,"amesisitiza Nsemwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Emil Kasagara amebainisha mkoa wa Mwanza umejipanga vizuri kufanikisha wiki hiyo ya kitaifa ya maziwa kwa kushirikiana na bodi ya maziwa na kuwataka wananchi kutumia vizuri fursa hiyo.
Maadhimisho hayo ya 27 yanayofanyika kila mwaka mwishoni mwa Mei na kuhitimishwa Juni Mosi,mwaka jana yalifanyika Mkoani Tabora.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.