RAS Balandya awataka Maafisa Mazingira kuwa wabunifu wa utunzaji na kuyalinda Mazingira
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg.Balandya Elikana amewataka Maafisa Mazingira wa Mikoa na Halmashauri Kanda ya Ziwa kutumia vizuri elimu wanayopata kuhusu Mazingira kuja na mikakati kabambe ya utunzaji na kuyalinda kwa faida ya vizazi vijavyo.
Akizungumza leo kwa niaba yake kwenye ufunguzi wa Warsha ya Kikanda ya kukuza uelewa kuhusu mpango wa Hifadhi na usimamizi wa Mazingira mwaka 2022-2023,Katibu Tawala Msaidizi,Mpango na Uratibu,Ndg.Joachim Otaru amesema kumekuwepo na kasi ya uharibifu wa Mazingira kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini,hivyo ni wajibu kwa Maafisa Mazingira kuonesha matokeo chanya kupitia elimu wanayopata kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Otaru amebainisha Mkoa kama wa Mwanza bado utupaji wa taka ngumu kwenye Ziwa Victoria imezidi kuongezeka na shughuli za Kilimo kando kando ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ya maziwa na mito,yote hayo yanahitaji kufanyiwa kazi kupitia njia mbalimbali ili wananchi waelimike vizuri.
"Niipongeze Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwaleta Wataalamu wake hapa Mwanza na kutoa elimu hii,Ziwa letu Victoria kuna mambo mengi ya hovyo yanayofanyika ukiwemo Uvuvi haramu,niwaombe Maafisa Mazingira punguzeni muda mwingi wa kukaa Ofisini badala yake fanyeni kazi kwenye maeneo hayo yaliyopo kwenye tishio la uharibifu",Otaru
"Njia mojawapo ya kuwa na Mazingira bora na salama ni kama hii ya utoaji wa elimu,tusirudi nyuma kuwaelimisha wananchi wetu,changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi yanachangiwa na sisi wenyewe kama ukataji wa hovyo wa miti",Martha Kalowela,Afisa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Naye Afisa Mazingira kutoka Geita,Tito Mlela amesema elimu kama hiyo inazidi kuwaongezea uwezo na wao kupata nafasi ya kuwasilisha baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo utungwaji wa Sheria ndogo ndogo ili ziwasaidie kutekeleza majukumu yao.
"Mkoa ninao toka una shughuli nyingi za uchimbaji wa Madini,sehemu hizo uharibifu wa Mazingira ni wa kiwango cha juu,naamini baada ya Warsha hii nitapata la kujifunza ambalo kitakuwa na tija eneo langu la kazi.
Warsha hiyo imewashirikisha Maafisa Mazingira wa Mikoa na Halmashauri kutoka Mikoa ya Mwanza,Geita,Simiyu,Mara na Kagera.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.