Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana amewakumbusha Maafisa Tarafa Kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria pia kutambua Fursa zinazopatikana katika maeneo ya kazi zao.
Ndg. Balandya amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya uongozi kwa Maafisa Tarafa ambayo yanaongozwa na Maafisa Tarafa wawili waliochaguliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Desemba 16, 2022 kwenda kushiriki Mafunzo hayo jijini Dodoma.
"Ni muhimu sana tukawatumikie wananchi kwa kutoa huduma bora kama ilivyo ainishwa katika waraka Na.1 wa Mwaka 2017 wa maendeleo ya utumishi na kuona fursa zinazopatikana katika maeneo yetu kwakuwa sisi Maafisa Tarafa ndio wasimamizi wa mambo yote ya Serikali haswa katika ngazi ya chini ya uongozi,"
" Matarajio yangu ni kwamba mafunzo haya yatawasaidia sana katika kuwajenga kimaadili kiuzalendo na kuwaandaa kuwa tayari kutoa huduma kwa wananchi tunaowatumikia na kuleta matokeo chanya kwa Serikali ya Mkoa," Amesema Mtendaji huyo wa Mkoa
Naye Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu Daniel Machunda amesema mafunzo yatakayotolewa kwa Maafisa hao yanalenga kuwakumbusha wajibu wao katika kazi.
"Mafunzo haya yanayotolewa kwenu yanahusisha mada muhimu ikiwa ni pamoja na masuala ambayo nyinyi kama watumishi wa umma mnapaswa kufanya au hapaswi kufanya kwa mujibu wa sheria na kanuni,"
"Napenda kutumia fursa hii kuwaambia Maafisa Tarafa wote kwa pamoja tunaouwezo wa kufanya maajabu na kufanya Mkoa wetu wa Mwanza ambao ni wa kimkakati kuwa kinara na Mikoa mingine ikaiga kutoka kwetu kutokana na utendaji wetu," Amesema. Machunda.
Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha Maafisa Tarafa kufahamu dira, dhima na malengo Ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pia kufahamu haki, wajibu na majukumu yao kama watumishi wa Umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.