MAAFISA UANDIKISHAJI MWANZA WATAKIWA KUSIMAMIA UBORESHAJI WA DAFTARI KWA WELEDI
Mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele amewataka Maafisa Uandikishaji watakaohusika kwenye uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kusimamia zoezi hilo kwa weledi ili kuleta ufanisi.
Jaji Mwambegele amesema katika kufanikisha zoezi la uboreshaji wa daftari hilo ni lazima kufuata sheria za tume huru ya uchaguzi mathalani zinazosimamia uandikishaji wa wanachama wapya na uboreshaji wa taarifa kwa wanachama waliokuwepo na si vinginevyo.
Jaji huyo wa Mahakama ya Rufaa ametoa rai hiyo mapema leo Agosti 10, 2024 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa watendaji ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura yanayofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
"Ni muhimu kuyaekeleza majukumu yenu kwa umakini hususani kwenye utunzaji wa vifaa ambavyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vitatumika katika maeneo yote ya uboreshaji nchini hivyo ni lazima tukashirikiane kwenye hilo". Amesema Jaji Mwambegele.
Vilevile, amefafanua kuwa mafunzo hayo yatahusisha ujazaji wa fomu mbalimbali za kujiandikisha pamoja na matumizi ya vifaa vya bayometriki na kwa pamoja yatawapa uwezo wa kwenda kusimamia zoezi hilo katika ngazi za kata na uboreshaji kwa ujumla.
Awali, Hakimu Mkazi Mwandamizi kitoka Wilaya ya Ilemela Christian Mwalimu aliwaapisha maafisa uandikishaji wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambao kwa pamoja waliapa kutunza siri pamoja na kiapo cha kujitoa kwenye vyama vya siasa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.