MACHINGA MKOA WA MWANZA HATUTAANDAMANA : MWENYEKITI SHIUMA
Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Mkoa wa Mwanza (CHIUMA) Mohamed Dauda amesema wafanyabiashara wadogo Mkoa huo (Machinga) hawataandamana Janauri 24, 2024 kama inavyohamasishwa na vyama vya siasa.
Dauda ametoa tamko hilo mapema leo tarehe 22, Januari 2024 wakati wa mkutano wa shirikisho hilo pamoja na waandishi wa Habari uliofanyika kwenye Stendi ya Mabasi Nyegezi.
Amesema, kundi hilo linalojipatia kipato kupitia biashara ndogondogo halipo tayari kutumiwa na wanasiasa kwani wataathiri biashara zao kwa kujihusisha na uvunjifu wa amani.
Amesema kundi hilo wanamshukuru Rais Samia kwa kuwawekea mazingira rafiki ya kazi kwa kuwajengea Ofisi nchi nzima na kuwatengea maeneo na kwamba imekua ni fursa sahihi ya kukuza kipato na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Ameendelea kufafanua kwamba hakuna machinga atakayeandamana mkoa mzima na yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kuondolewa kwenye shirikisho lao mara moja.
Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Venatus Anatory ametumia wasaa huo kuhamasisha bodaboda kujikinga na janga la Kipindupindu na akatoa wito kwao kuweka vibeba taka kwenye maeneo yao na kuhakikisha wananawa maji tiririka.
"Hoja zetu na Serikali ya Rais Samia zinaishia mezani, hatuna sababu ya kuandamana maana hata tulipokutana naye Dodoma alitusikiliza na tuna furaha kwani tunafanya biashara kwa uhuru hatubughudhiwi na mtu." Katibu Mkuu.
Naye Beatrice Mgema, mfanyabiashara kwenye Stendi ya Nyegezi amebainisha kuwa Rais Samia ni kama mlezi wa biashara zao kwani amewawekea mazingira mazuri ya kazi na kwamba riziki wapatazo hawako tayari kuharibu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.