Chama cha Madereva Mkoa wa Mwanza na kile cha Wamiliki wa Mabasi (TABOA) kwa pamoja wameiomba serikali kutunga na kutilia mkazo kanuni na sheria zitakazowabana abiria ambao hawafuati sheria za barabarani.
Hayo yamesemwa mkoani Mwanza katika mkutano ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) uliolenga kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa usafirishaji juu ya rasimu mpya ya kanuni na sheria za sekta hiyo nchini.
Akizungumuza kwa niaba ya wanachama wa chama cha madereva Mkoa wa Mwanza Salim Iddy, alisema kwa muda mrefu sasa sheria na kanuni za usalama barabarani zinazotungwa zimekuwa zikilenga zaidi kuwabana madereva huku zikiwaacha abiria wakifanya wanavyotaka.
“Kuna wakati unakuta abiria wanapanda kwenye mabasi wakiwa wamelewa au hata na chupa za vilevi wanakuwa wasumbufu toka mwanzo hadi mwisho wa safari, kiasi cha kusababisha dereva kuendesha bila amani na hata kumfanya apoteze umakini wakati wa safari.
“Pia wapo abiria wanapenda kusimama maeneo yasiyokuwa na vituo vya daladala lakini dereva anapowachukua yeye ndiyo anapigwa faini, tunaziomba mamlaka zinazohusika ziwachukulie na wao hatua kwani wao ndiyo chanzo cha uvunjifu wa sheria za barabarani,” alisema Iddy.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha wamiliki wa mabasi Mkoa wa Mwanza, Anwar Said, aliongeza kuwa kuna haja ya serikali na vyombo vinavyohusika kuanza kuvibana kwanza vyombo vya usafiri vya umma ikiwemo mabasi ya mwendo kasi ili kuonyesha mfano kwa wengine.
“Suala la kudhibiti uzidishwaji wa abiria kwenye vyombo vya usafiri limekuwa likilenga zaidi mabasi yanayomilikiwa na watu binafsi, serikali inatakiwa ianze na mabasi ya mwendo kasi ambayo yanabeba abiria kupita kiwango.
“Pia waendeshaji wa magari ya serikali mara nyingi wanatumia mwendo mkubwa kuliko kawaida lakini cha kushangaza hakuna hatua zinazochukuliwa huku madereva wetu wakizidisha mwendo kidogo tu mnawakamata mnawapiga faini, huo ni uonevu kwa kuwa sheria ni zetu sote.
“Hivi sasa pia tunashuhudia ongezeko na utitiri wa mamlaka zinazodhibiti vyombo vya usafiri nchini tunaiomba serikali iliangalie hili na kama itawezekana zipunguzwe, kwani kadri mamlaka zinavyozidi kuwa nyingi ndio mianya ya rushwa inaongezeka kutoka kwa madereva na wafanyakazi wetu, alisema Anwar.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.