Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe, Mhandisi Robert Gabriel amewakumbusha Wananchi Mkoani humo kuzingatia afya zao mara kwa mara wakati Serikali ya awamu ya Sita ikiendelea kuwajengea Vituo vya Afya karibu na maeneo yao.
Akizungumza na Wananchi Wilayani Magu wakati wa kukabidhiwa Vituo vya afya vitano,Mhandisi Gabriel amesema nguvu kazi inakwenda pamoja na Wananchi wenye afya hivyo ni wajibu wa kila mmoja kutumia fursa hiyo kujiaminisha na afya yake.
"Haitakuwa na maana Serikali hii kutoa fedha nyingi kuboresha huduma za afya halafu kuwepo na vifo vya Mama wajawazito au Wananchi kutaabika na maradhi tujifunze kutumia maarifa ya huduma hizi" amesisitiza mkuu huyo wa Mkoa.
Wilaya ya Magu imemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Vituo vitano vya Afya vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 950.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe,Salum Kalli amesema kuwepo kwa Vituo hivyo vya afya vimempunguzia mwananchi kutembea mwendo mrefu kusaka huduma hiyo.
"Kuwepo karibu Vituo vya afya kwa kiasi kikubwa kunampa fursa mwananchi kupata matibabu bora na ya haraka na kuendelea na shughuli zake za Maendeleo" amesema Mkuu huyo wa Wilaya ya Magu.
Akitoa taarifa fupi ya huduma za afya Mkoani Mwanza,Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Thomas Rutachunzibwa amesema mpango uliopo sasa ni kuboresha huduma za afya kwa kujenga Hospitali kwenye Wilaya zote za Mkoa huo,kujenga Wodi ya Wagonjwa wa Saratani Hospitali ya Bugando itakayogharimu Bilioni 5, pamoja na uwekaji wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa Maradhi.
Mkoa wa Mwanza umepokea Shilingi Bilioni 40 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ambapo ujenzi wa Vituo vya afya na uwekaji wa vifaa vya kisasa vya kufanyia uchunguzi wa Maradhi mbalimbali unaendelea kufanyika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.