Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameumaliza mgogoro wa bei uliokuwepo baina ya wakulima wa zao la pamba nchini na wanunuzi, ambapo sasa zao la pamba litaendelea kununuliwa kwa bei elekezi ya serikali ya sh. 1,200 kwa kilo.
Waziri Mkuu aliumaliza mgogoro huo mara baada ya kukutana na makundi ya wanunuzi na wakulima, wakuu wa mikoa/wilaya na wakurugenzi watendaji kutoka kwenye mikoa inayolima pamba nchini wakati wa mkutano wa dharula wa wadau wa tasnia ya pamba nchini.
Alisema katika kukithamini kilimo cha pamba, Serikali iliitisha vikao vingi tangu mwaka jana kwa ajili ya kuimarisha zao hilo na kwamba dhamira yake ni kuona kilimo cha pamba kinamnufaisha mkulima.
Alisema hatua hio imeleta mafanikio ya uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 222,000 kwa msimu uliopita wa kilimo hadi kufikia karibu tani 450,000 kwa msimu wa mwaka huu na aliwahakikishia wakulima kuwa pamba yote iliyozalishwa kwa msimu huu itanunuliwa yote.
Aliwataka wakuu wa mikoa na wilaya, wakurugenzi watendaji kwenye maeneo kuangalia utaratibu mzuri wa kuwasaidia wanunuzi ili kuhakikisha pamba yote inayonunuliwa kutoka kwa mkulima inawafikia salama.
“ Aidha muweze kujiridhisha na mifumo ya fedha iliyopo kama iko sawa ili wakulima wetu waweze kulipwa fedha zao kupitia benki, alisema na kuwashukuru wanunuzi wa pamba kwa kuitikia mwito wa serikali kwa kununua pamba kwa bei elekezi ya serikali.
Aliziagiza Kamati za ulinzi na usalama za wilaya na mkoa kuwahakikishia wanunuzi na wakulima usalama wa fedha zao mara baada ya kuuza na kununua pamba ili kuhakikisha pande zote mbili zinakuwa salama.
“Lengo letu kama serikali kama serikali ni kuhakikisha mwenendo wa manunuzi unakwenda vizuri,” alisema na kuwahakikishia wanunuzi kuwa biashara yao itasimamiwa vizuri.
Kwa upande wa ubora wa pamba, alisema mkakati uliopo wa serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa inaimarisha ubora wa zao la pamba kwa kuwawezesha wakulima kulima kilimo chenye tija kwenye maeneo yao.
Alisema mkakati huo utakwenda sanjari na viongozi na watalaam wa zao hilo kuwaelimisha wakulima juu ya ubora wa zao hilo ili hata baada ya mavuno, wasichanganye maji na mchanga kwa ajili ya kuongeza uzito ili kujipatia fedha, jambo ambalo litasababisha bei ya pamba kushuka kwenye soko la dunia.
“ Pamba kukosa ubora, wakati mwingine unasababishwa na wakulima kukosa sehemu ya kuhifadhia pamba yao, niwaombe viongozi mjiridhishe kwenye maeneo yenu kama pamba ina ubora unaotakiwa,” alisema na kuwataka viongozi kuzihakiki mizani zinazotumika kununulia pamba ili kubaini zenye kasoro na hatua zichukuliwe kwa wanunuzi wenye mizani za kumpunja mkulima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.