MAJALIWA AWATAKA WANAWAKE KUTUMIA MITANDAO YA KIJAMII KUJIIMARISHA KIBIASHARA
Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (MB) ametoa wito kwa wananwake nchini kutumia Mitandao ya kijamii kutangaza biashara na ubunifu wao ili kujiimarisha na kukuza mitaji yao kwa kuongeza wigo wa wateja wanaopatikana kwa haraka.
Ametoa wito huo leo jioni Mei 18, 2024 kwenye hafla ya Kuwatunuku Wanawake wanaojishughulisha kuinua uchumi wao kupitia kazi mbambali zilizopewa jina la Malkia wa nguvu chini ya usimamizi wa Clouds Media Group zilizofanyika katika ukumbi wa Kwatunza Beach wilayani Ilemela.
Aidha, amesema kuwa Kaulimbiu ya Tuzo hizo isemayo 'Weka Tuweke' inaakisi uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais Samia kwenye miradi hivyo amewataka wanawake kutumia kikamilifu fursa zilizopo nchini kwani tayari Serikali imeweka mifumo ya kurahisisha uwekezaji nchini.
Amebainisha pia hatua zinazofanywa na Serikali kuboresha mifumo ya kuwainua wanawake na kuboresha shughuli zao za uchumi za kila siku kama Elimu ambapo hivi sasa vijana wengi wa kike wanapata elimu bila vikwazo kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu pamoja na huduma za afya zinazoenda sambamba na uimarishaji wa upatikanaji wa maji safi.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewashukuru Clouds Media Group kwa kuchagua Mkoa wa Mwanza kufanyika tukio kubwa la kutoa tuzo kwa wanawake walioonesha juhudi kubwa katika kujiletea maendeleo kwani ugeni huo utachagiza maendeleo ya Mkoa.
Aidha, amebainisha uwepo wa miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa kama Meli ya MV Mwanza kwa zaidi ya Bilioni 110, Bilioni 28 zinazojenga Vivuko vitano, zaidi ya Bilioni 12 zinazokarabati Uwanja wa ndege, Bilioni 71 zinazojenga mradi wa Maji Butimba na kwamba Mwanza inachangia asilimia 7.1 ya Pato la Taifa.
"Mwaka wa 8 sasa tumeratibu hamasa, sherehe kwa wanawake na kupeana moyo kwenye mageuzi ya kukuza nguvu kupitia mradi wa Malkia wa nguvu na imesaidia kuwajaza ujasiri wanawake wote nchini." Lilian Masuka, Mwenyekiti Kamati ya Malkia wa nguvu.
Clouds media Group kwa mwaka huu 2024 imekuja kaulimbiu ya 'Weka Tuweke' ikimaanisha kuwatia moyo wanawake kujiamini na kuwekeza ili jamii inayowazunguka nayo iwekeze kwao katika kuboresha bidhaa zao na kuinua uchumi na wanatarajia kugusa zaidi ya wanawake milioni 5 ndani ya miezi 8.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.