MAKALLA AAGIZA MPANGO KAZI WA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA UKIMWI MWANZA
*Aagiza kubaini sababu za maambukizi makubwa na kuwekwa kwa mikakati ya kuondoa*
*Amemshukuru Rais Samia kwa kuboresha huduma za Afya*
*Aagiza kukomeshwa kwa mila potofu zinazochochea Maambukizi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wadau wa Afya kuweka Mpango Kazi madhubuti wa kupunguza Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI mkoani humo.
Mhe. Makalla ametoa agizo hilo leo tarehe 07 Mei, 2023 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati akifungua kikao kazi cha Afua za UKIMWI kilichowakutamisha Wadau mbalimbali kutoka kwenye wilaya zote za Mkoa huo.
Mhe. Makalla amesema ni wajibu wa wadau wote wa Kikao hicho kuweka Mikakati ya kujua nini sababu ya kuwa na kiwango kikubwa cha Maambukizi hadi kushika nafasi ya nne Kitaifa na amewataka kutafiti sababu zilizopelekea hali hiyo na waandae Mpango kazi wa kuwatoa huko.
"Kwa takwimu hizi za kwamba Kiwango cha Kitaifa kuna Maambukizi kwa asilimia 4.7 na Mwanza kuwa na asilimia 7.2 huku wenzetu wanaotuzunguka kama Geita na Mara wakiwa na asilimia 5 huku Simiyu 3.9 na tunaambiwa hadi kufikia Mwezi Mei 2023 tumekuwa na idadi ya watu 127650 wanaotumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi, hali ni mbaya na tusiikubali", amesisitiza CPA Makalla.
Akimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutoa matibabu bure kwa waathirika, kuimarisha Afya ya msingi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuweka mazingira wezeshi amewataka wananchi kuachana na Mila na desturi mbaya kama ndoa za utotoni amewataka kuitikia wito wa kufanya tohara kwa wanaume na kuelimisha rika la vijana ili kupambana na Maambukizi mapya.
Vilevile, ametumia wasaa huo kulishukuru Shirika la ICAP na wadau wengine wote wanaoshirikiana na Serikali katika kuweka Afua mbalimbali za kuondoa Maambukizi ya virudi vya UKIMWI nchini huku akitoa wito kwa wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo ili kuilinda Tanzania.
Naibu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la ICAP nchini, Dkt. John Kalemele ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuweka mazingira wezeshi na yenye ushirikiano katika kufanikisha shughuli za Afua za Ukimwi nchini.
"Sasa hivi tuna watu wanaotumia dawa za kufubaza Maambukizi ya Upungufu wa kinga Mwilini (UKIMWI) wapatao Laki na Ishirini na hiyo yote inafanikiwa kutokana na mazingira wezeshi yanayowekwa na Serikali na kwa mkoa wa Mwanza tunawashukuru sana serikali ya mkoa kwa ushirikiano. "
Vilevile, amebainisha kuwa katika kutekeleza afua za kutokomeza Maambukizi ya UKIMWI wamekuwa wakijihusisha na kufanya Tohara kwa wanaume na shunguli za Uelimishaji rika hasa kwa makundi ya wasichana walio kwenye rika Balehe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.