Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Mhe. Abdurahman Kinana, ameridhishwa na namna ujenzi wa miradi ya kimkakati inavyoendelea Mkoa wa Mwanza kwa hatua iliyofikiwa na usimamizi wa miradi hiyo.
Mhe.Kinana ameyasema hayo mara baada ya kuwasili Mkoa wa Mwanza akitokea Mkoani Geita na kukuta ujenzi ukiendelea ndipo alipowasilisha salaam za Mhe.Rais akizungumza na wananchi, wataalamu na viongozi mbalimbali katika Mradi wa Daraja la J.P MAGUFULI lenye urefu wa km 3.2 linalojengwa na mkandarasi Kampani ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC ) kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 700 na kutarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2024, ndipo alipowataka watendaji kuendelea kusimamia miradi hiyo kwa weledi na ubora.
"Mhe.Rais amenituma niwasalimie,na anangoja aje kuwa Mgeni Rasmi kufungua daraja hili,na siku ya kufungua daraja hili watachinjwa ng'ombe wengi sana, na siyo ng'ombe tu ng'ombe lazima aende na kinywaji,''alisema Mhe.Kinana.
Aidha, Mhe.Kinana aliongeza furaha yake alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali na wanachama wa chama cha Mapinduzi alipowasili Ofisi ya CCM Mkoa ambapo aliwashukuru wote kwa mapokezi mazuri na jinsi walivyomlaki na walivyojitokeza kwa wingi.
Vilevile Mhe.Kinana amekagua ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza Hapa Kazi tu mradi unajengwa kwa Gharama ya Shilingi Bilioni 97 na kuridhika namna mradi huo unavyoendelea.
Pamoja na kukagua uhai wa Chama cha Mapinduzi kwa kuzungumza na wanachama wa Chama hicho pamoja na wavuvi na vikundi vyao, Mhe.Kinana amekagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020/2025 kwa kutembelea mradi wa Soko Kuu Jijini hapo unajengwa na Kampuni ya Mohamed Builders Co.Ltd kwa gharama ya Shilingi Bilioni 20 huku ukitarajia kunufaisha wafanyabishara wakubwa na wadogo.
Hata hivyo, Mhe.Kinana aliwasili Mwanza Septemba 4, 2022 na kupokelewa katika Kijiji cha Igaka, Kata ya Buzilasonga wilayani Sengerema mkoani Mwanza, huku akilakiwa na viongozi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Mwanza Mhe. Dkt. Athony Dialo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima, wanachama na wananchi wa Mkoa huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.