*Dkt. Mpango kufanya ziara ya kikazi Mwanza kwa siku tatu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Kighoma Malima anawakaribisha wananchi wote wa Mwanza na Mikoa ya Jirani kumpokea na kumlaki Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango anayetarajia kuwasili siku ya Jumatatu tarehe 12/09/2022 majira ya saa 9 alasiri.
Amesema hayo mapema leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa alipokua akizungumza na waandishi wa Habari kufuatia ugeni huo Mkubwa wa Kitaifa kwa ziara ya kikazi ya siku 3 Mkoani humo.
"Naomba wakaazi wa Mwanza tuoneshe Uzalendo mkubwa kwa kumpokea mgeni wetu tukiishukuru Serikali kwa kazi kubwa ya kuwaletea Maendeleo wananchi na kwenye hilo naomba tujitokeze kwa wingi kwenye kumlaki kandokando ya barabara kuanzia Airport, Pasiansi, Rock City na maeneo yote ya miradi ambayo Mhe. Makamu wa Rais atakagua." Amesema Malima.
Mhe Malima amesema mnamo tarehe 13/09/2022 Makamu wa Rais atazindua jengo la huduma za Kansa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na baadae kwenye siku hiyohiyo ataelekea kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure ambapo atazindua Huduma za Mama na Mtoto kwenye jengo Maalum la Kisasa.
Aidha, ndani ya Siku ya tarehe 13, 09, 2022 Mhe Makamu wa Rais atazindua Stendi ya Kisasa ya Mabasi na maegesho ya malori Nyamhongolo ambayo inakuja kumaliza tatizo la msongamano wa magari na kusaidia kuongeza mapato kwenye Halmashauri ya Ilemela kwani inakusudia kukusanya zaidi ya Bilioni 2 kwa mwaka.
Vilevile, Mhe Malima amesema siku ya Tarehe 14/09/2022Mhe. Makamu wa Rais ataweka Jiwe la Msingi katika mradi wa ujenzi wa Chanzo cha Maji Butimba ambao unatarajiwa kuzalisha lita milioni 48 kwa siku na kwamba uwekezaji huo wa zaidi ya Bilioni 70 utasaidia kupunguza uhaba wa maji kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo ya jirani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.