MAMLAKA ZA HALI YA HEWA BARANI AFRIKA ZATAKIWA KUTOA TAARIFA ZITAKAZOWASAIDIA WANANCHI KUJIEPUSHA NA MAJANGA
Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ametoa wito kwa Mamlaka za hali ya hewa barani Afrika kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa hususani za rada ili kuwaepusha wakulima, wavuvi na wananchi na majanga yanayoepukika.
Waziri Mbarawa ametoa wito huo mapema leo Agosti 26, 2024 wakati akifungua mafunzo ya siku 5 kwa Mataifa 13 kutoka barani Afrika yaliyodhaminiwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) yanayofanyika kwenye hoteli ya Malaika Mkoani Mwanza.
Prof. Mbarawa amesema, tahadhari kutoka mamlaka za hali ya hewa hususani za rada zinategemewa sana na wananchi wanaojihusisha na shughuli za uvuvi na kilimo ambao wanahitaji kujua wanapoamka asubuhi watakua na hali gani itakayowaruhusu kwenda kwenye shughuli zao.
"Ninayo imani kuwa kupitia mafunzo haya washiriki wataimarika kwenye utumiaji wa teknolojia na utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa hususani za rada na itasaidia kuinua uchumi wa nchi na kuiepusha jamii na majanga kama ya kimbunga kwenye maziwa na bahari kwa wavuvi." Amesema Prof Mbarawa.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bwana Balandya Elikana amewataka nchi washiriki wa mafunzo hayo kutumia mafunzo hayo kuboresha huduma kwenye mamlaka zao hususani utoaji wa haraka wa utabiri wa hali ya hewa.
Vilevile, amewataka kuhakikisha wanabadilishana uzoefu wa namna bora ya kuendesha mamlaka hizo katika kuwahudumia wakulima, wavuvi na wafugaji ambao wanategemea zaidi taarifa za hali ya hewa kwenye shughuli zao za uchumi.
"Mkoa wa Mwanza una zaidi ya wananchi milioni tatu kwa mujibu wa sensa ya hivi karibuni na unashika nafasi ya pili kwenye uchangiaji wa pato la Taifa hivyo wachimbaji wa madini, wakulima na wavuvi ni lazima wapate taarifa sahihi za utabiri wa hali hewa kabla hawajaingia kwenye shughuli zao." RAS Elikana.
Aidha, ametumia wasaa huo kuwakaribisha washiriki kutembelea vivutio vya utalii kwenye mkoani humo hususani Hifadhi ya Taifa Saanane na kituo cha Bujora na akawakaribisha wawekezaji mkoani humo kwani fursa ni nyingi za kuwekeza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.