Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Daniel Machunda leo Januari 15, 2025 amefungua kikao kazi cha kupokea maoni ya wadau kuhusu utafiti wa sekta ndogo ya usafiri wa majini kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kuwakutanisha wadau kutoka mikoa inayozungukwa na maziwa, bahari na mito.

Bw. Machunda amesema serikali imejipanga kikamilifu kuyafanyia kazi maoni yatakayokusanywa ili kuboresha usalama, ufanisi na mchango wa sekta ya usafiri wa majini katika kukuza uchumi wa taifa, akisisitiza kuwa rasilimali za maji ya ndani na bahari ni miongoni mwa nguzo muhimu za ongezeko la pato la taifa.

Ameongeza kwa kusisitiza kuwa Kikao kazi hicho ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kuhakikisha sekta ya usafiri wa majini na uchumi wa buluu vinakuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwakilishi wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Johnson Laizer, amepongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kuweka mazingira wezeshi yatakayohakikisha maoni ya wadau yanapatikana kwa uwazi na ushirikishwaji mpana.

Aidha amesema sekta ya uchumi wa buluu inagusa maisha ya wananchi wa hali zote, kuanzia wavuvi, wafanyabiashara, wasafirishaji hadi watumiaji wa huduma za usafiri wa majini, na kwamba maendeleo ya sekta hiyo yana mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Nao wadau walioshiriki kikao hicho wameeleza kuwa ukusanyaji wa maoni ya nchi nzima utasaidia kuboresha sera, sheria na mikakati itakayochochea maendeleo endelevu ya sekta ya usafiri wa majini.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.