Mapambano dhidi ya ukatili na mimba za watoto shuleni katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza yameoneka kutokuwa mafanikio chanya baada ya takwimu kuonyesha kuongezeka kila mwaka.
Hayo yamebainishwa jijini Mwanza katika semina iliyoandaliwa na Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto (KIVULINI) kwa taasisi mbalimbali zikiwamo ya mwendesha mashitaka mkoa, mahakama, askari wa dawati la jinsia, wapelelezi, ustawi wa jamii na mashirika binafsi yanayojihusisha na utetezi wa haki za binadamu, uzuiaji wa vitendo vya ukatili.
Akiwasilisha taarifa za matukio ya ukatili na mimba za watoto , Mkuu wa dawati la Jinsia kutoka Polisi Mkoa wa Mwanza, Berth Shija alisema mwaka 2017 walipokea kesi 1,287 na zilizofikishwa kitengo cha upelelezi ni 1,200 ambapo 9 zilikosa ushahidi.
Alisema kati ya kesi 1,200 zilizokuwa zikifanyiwa upelelezi, kesi 59 ndizo zilifikishwa mahakamani na kati ya hizo 19 ndiyo zilifanikiwa.
“Mwaka 2018 taarifa zilizopokelewa ni 1,682, zilizofika kitengo cha upelelezi ni 1,263, zilizokosa ushahidi 142 na zilizofikishwa mahakamani 278 lakini kati ya hizo zilizofanikiwa kwa kupata ushindi mahakamani ni 36 pekee.
“Mwaka huu 2018 kuanzia Januari mpaka sasa tumepokea kesi 1,012, zilizofikishwa kwenye upelelezi 827, zilizokosa ushahidi ni sita ambapo zilizofikishwa mahakani 179 na hatujaweza kujumlisha kwani hatujapokea taarifa kutoka wilaya zote za mkoa wetu wa Mwanza,”alisema Shija.
Kwa upande wa Mkuu wa Dawati la Jinsia kituo cha Polisi Kirumba, Rico Ndaro alisema matukio ya mimba kwa wananfunzi kuanzia mwaka 2016 yalikuwa 17 lakini 2017 yalikuwa 31, 2018 yalikuwa 41 ambapo kwa mwaka huu yamepokelewa 28 kati ya Januari hadi Juni.
“Kwa miaka mitatu iliyopita jumla ya kesi 96 ziliripotiwa kituo cha polisa kirumba na kesi 44 zilifikishwa mahakamani ambapo kati ya hizo 21 zilishinda mahakamani ambapo katika kesi hizo watuhumiwa 18 walifungwa kila mmoja miaka 30 jela.
“ Watuhumiwa wengine wawili walifungwa kifungo cha maisha jela na mmoja alifungwa miaka 35 jela ambapo jumla ya kesi 23 ziliondolewa mahakamani kwa kukosa ushahidi.
“Kati ya kesi 96 zilizopokelewa Kirumba, kesi 52 ziliishia polisi kwa kukosa ushahidi lakini jumla ya kesi 36 zilitokea hasa katika maeneo ya Igombe na Kayenze Wilaya ya Ilemela,”alisema.
Wakichangia mada ya mkakati wa kukomesha vitendo hivyo na kufanikisha kesi hizo, wadau mbalimbali walionekana kulalamikia kitengo cha upelelezi na madaktari kushindwa kujaza vizuri fomu namba 3 ya polisi (PF3) na kutofika mahakamani ili kutoa ushahidi.
Mrema Juma kutoka kutoka ofisi ya mpelelezi Wilaya ya Ilemela alisema ni kweli baadhi ya kesi zinaishia hapo au kukaa muda mrefu kutokana na kukosa ushirikiano na watu ambao ni wahusika hivyo aliwataka wadau wote wanaohusika na mlolongo wote wa kufanikisha kesi hizo kushirikiana.
Baadhi ya madaktari waliochangia walisema kuwa si wote wanaokataa kwenda mahakamani kutoa ushauri isipokuwa wachache wanaokwenda hupata usumbufu mkubwa kutoka kwa mahakimu kwa kukaa muda mrefu na hata kesi kuahirishwa bila kuitwa.
Pamoja na michango yao, waliiomba mahakama kuanza na kesi za mimba na ukatili kwanza ili kuwapa nafasi ya kuwahi kurudi katika majukumu yao ya kuwahudumia wananchi katika maeneo yao ya kazi badala ya kusota mahakamani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.